2017-09-25 11:09:00

Mgogoro wa Korea ya Kaskazini unahitaji uamuzi wa Jumuiya ya Kimataifa


Vatican ni kati ya nchi kadhaa duniani ambazo hivi karibuni katika mkutano wa 72 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa zimeridhia Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku Silaha za Kinyuklia ili kuendeleza mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani unaofumbatwa katika: Uhai, utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni mkataba unaopania kukuza na kudumisha ushirikiano unaowajibisha; majadiliano katika ukweli na uwazi; uaminifu na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Vatican katika masuala ya ushirikiano wa kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wakati wa maadhimisho ya utiaji mkwaju kwenye mkataba huu wa kimataifa amewataka wajumbe kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kutekeleza yaliyomo kwenye mkataba huu, ili dunia iweze kuondokana na hofu pamoja na wasiwasi wa mashambulizi ya silaha ya kinyuklia. Hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kuhakikisha kwamba, inaunda mazingira yenye ulinzi na usalama pasi na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia.

Huu ni wakati wa kutafakari kwa kina na mapana kanuni maadili ya amani, ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kuheshimiana, kuthaminiana na kuaminiana katika maamuzi na utekelezaji wa vipaumbele vinavyotolewa na Jumuiya ya Kimataifa. Malumbano ya kijeshi, vitisho vya mashambulizi ya silaha kali za kinyuklia; majaribio ya utengenezaji na ulipuaji wa makombora ya masafa marefu duniani na vita ya maneno kati ya Marekani na Korea ya Kusini ni vitisho dhidi ya utamaduni wa amani na utulivu; ustawi na maendeleo ya wengi; tunu msingi zinazopewa kipaumbele kwa sasa na Jumuiya ya Kimataifa.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican, baada ya uzinduzi wa Kitabu kilichoandikwa na kuhaririwa na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi kinachokwenda kwa jina la “The Vatican in the Family of Nations”  kinachoonesha mchango wa Vatican katika Jumuiya ya Kimataifa anasema: Diplomasia ya Vatican katika Jumuiya ya Kimataifa ni kwa ajili ya huduma ya amani, haki msingi za binadamu, ustawi, mafao na maendeleo endelevu ya binadamu wote.

Kardinali Parolin anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wanaotaka kufanya maamuzi peke yao na kudhani kwamba, wao ndio wanaoshikilia hatima ya Jumuiya ya Kimataifa. Lakini, maamuzi mazito yanapaswa kutolewa na kutekelezwa kwa pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi. Vatican inapenda kukazia kwa namna ya pekee kabisa huduma makini ya maendeleo endelevu ya binadamu; kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; amani na maridhiano kati ya watu. Kardinali Parolin anakaza kusema, hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa dira na mwongozo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa amani, haki, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu.

Vita ya maneno na vitisho vya mashambulizi ya makombora ya masafa marefu kati ya Korea ya Kaskazini na Marekani ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa inayopaswa kuwa ni jukwaa la amani, upatanisho na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Leo hii, Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na mpasuko mkubwa katika medani mbali mbali za maisha, hali ambayo inahitaji majadiliano na upatanisho katika ukweli na uwazi, ili kurekebisha tofauti zilizopo na kuanza kushirikiana kama familia kubwa ya binadamu.

Hapa kuna umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa, ili kulinda na kudumisha amani, ustawi na maendeleo ya wengi; mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa kama changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa anasema Kardinali Pietro Parolin wanapaswa kuwajibika kikamilifu kwa kutambua kwamba, hatima ya maisha, ustawi na mafao ya wengi iko mikononi mwao, hivyo wanapaswa kuitafsiri dhamana hii katika matendo yanayoongozwa na busara, kanuni maadili na utu wema, tayari kutafuta na kudumisha amani na maendeleo endelevu duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.