Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Mchango wa diplomasia ya Vatican kwa familia ya binadamu ulimwenguni

Diplomasia ya Vatican inajikita katika huduma ya maendeleo endelevu; utu, heshima, haki msingi za binadamu, amani na utulivu! - AFP

25/09/2017 10:31

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi tangu mwaka 2002 hadi mwaka 2016 ametekeleza dhamana na wajibu wake kama Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss. “The Vatican in the Family of Nations” ni Kitabu ambacho kimeandikwa na kuhaririwa na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi ili kuonesha dhamana na mchango wa Vatican katika Familia ya binadamu kimataifa. Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican katika uzinduzi wa kitabu hiki, hapo tarehe 22 Septemba 2017 amesema, diplomasia ya Vatican na Kanisa katika ujumla wake, kimsingi inakazia kwa namna ya pekee kabisa: huduma makini ya maendeleo endelevu ya binadamu; kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani; elimu, afya, biashara, mawasiliano, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na haki miliki ya kiakili.

Kardinali Parolin anakaza kusema, hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa dira na mwongozo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa amani, haki, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. Hii ni sehemu muhimu sana ya utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Vatican katika masuala ya kidiplomasia inafuata kwa makini sana sheria, taratibu na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika kanuni maadili na ushirikiano unaosimamiwa na kuratibiwa na kanuni auni.

Baba Mtakatifu Francisko anasema upendo ni kanuni inayoshuhudia uaminifu wa Mama Kanisa katika huduma makini kwa binadamu inayosimikwa katika ukweli, umoja na mshikamano; chachu ya ujenzi wa madaraja yanayowaunganisha watu ili kuendeleza Injili ya matumaini kwa watu wa Mataifa. Diplomasia ya Vatican inafumbatwa katika mchakato wa uragibishaji wa maoni unaofumbatwa katika sauti ya kinabii inayopania kugusa dhamiri nyofu za watu, ili kukuza utu na heshima ya binadamu kwa kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha yake.

Kardinali Parolin anakaza kusema, ushirikiano wa kimataifa unaozungumziwa na Vatican unafumbatwa katika mahusiano ya kifamilia, shughuli za uchumi, utamaduni, siasa, haki na amani; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na upigaji rufuku wa utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi. Mwanadamu anapaswa kuwa ni kiini cha mchakato wa amani na utulivu duniani, kwa kudumisha upatanisho, msamaha na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Ndiyo maana hata Vatican katika mkutano wa 72 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, imeridhia Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku Silaha za Kinyuklia ili kuendeleza mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani unaofumbatwa katika: Uhai, utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kudumisha umoja na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kuliwezesha Kanisa kuendelea kuwa ni shuhuda na chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Kardinali Pietro Parolin anaendelea kufafanua kwamba, wanadiplomasia wa Vatican, tangu Mwenyeheri Paulo VI alipofungua malango ya Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, changamoto iliyovaliwa njuga na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, imeliwezesha Kanisa kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani. Kitabu hiki kinachambua sababu msingi zinazopelekea matukio mbali mbali duniani,  hatua zinazopaswa kuchukuliwa na suluhu yake katika Jumuiya ya Kimataifa! Kwa mfano kitabu hiki kinafafanua kwa kina mapana sababu kinazochangia umaskini wa hali na kipato; mmong’onyoko wa maadili na utu wema; athari za uharibifu wa mazingira; unyonyaji na uporaji wa rasilimali za dunia kwa mafao ya watu wachache ndani ya Jamii, mambo ambayo yanahatarisha sana amani, utulivu na mafungamano ya familia ya Mungu duniani.

Askofu Mkuu Silvano Maria Tomasi anafafanua matumaini ya familia ya Kimataifa katika mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030; umuhimu wa kumwilisha mapendekezo yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume kuhusu utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, Laidato si pamoja na kukoleza jitihada za ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vatican imekuwa mstari wa mbele kushiriki katika utekelezaji wa wa Mikataba na Itifaki za kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu duniani. Kitabu hiki ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa familia ya binadamu na kwamba, matumizi ya silaha duniani hayana hatima ya mwisho katika maisha ya watu. Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anatoa mwelekeo wa matumaini makubwa "Opus magnum” katika mchakato wa ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

25/09/2017 10:31