2017-09-25 09:56:00

Jumuiya ya Kimataifa ina dhamana ya kulinda uhuru wa kuabudu!


Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba, inalinda na kudumisha uhuru wa kidini na kuabudu kati ya watu wa Mataifa, na hasa zaidi, ikiwa waamini hawa ni sehemu ya makundi madogo madogo katika jamii ya watu! Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na umwagaji mkubwa wa damu ya watu wasiokuwa na hatia; nyanyaso za kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana; ghasia na vurugu; utekaji na uporaji wa rasilimali za watu; dhuluma, nyanyaso na ubaguzi wa kila aina pamoja na mauaji ya kimbari!

Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta chanzo kinachosababisha vitendo vyote hivi vinavyokwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, ili hatimaye, kukuza na kudumisha: utu wa binadamu, haki ya kuishi, uhuru wa dhamiri unaofumbatwa katika uhuru wa kidini. Waamini wa makundi madogo madogo ya kidini huko Mashariki ya Kati, ndio walioathirika kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni kadiri ya taarifa ya Mwaka 2016 iliyotolewa na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa Hitaji. Kati ya nchi 196 duniani, imebainika kwamba, nchi 38 zilikumbwa na ukosefu mkubwa wa uhuru wa kuabudu na kidini na kwamba, nchi 23 zilitumbukia katika dhuluma na nyanyaso za kidini duniani.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, wakati wa mkutano mkuu wa 72 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, huko, New York, Marekani, tarehe 22 Septemba 2017. Vitendo vya kigaidi, mauaji ya kimbari, utekaji na unyanyasi wa kijinsia; uporaji na uharibifu wa nyumba za ibada na makazi ya watawa; taasisi za elimu na afya zinazomilikiwa na mashirika ya kidini ni kati ya mambo ambayo yameathiri sana uhuru wa kuabudu na kwamba, wakristo duniani ni kati ya dini ambazo waamini wake wameathirika vibaya sana!

Askofu mkuu Gallagher anasema, kuna haja kwa viongozi waliopewa dhamana ya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba: wanalinda na kudumisha haki msingi za binadamu; wanawalinda raia na mali zao; utu na heshima yao kama binadamu na kwamba, mauaji ya kimbari kwa misingi ya kidini ni jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika na Jumuiya ya Kimataifa. Changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa huko Mashariki ya Kati ni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Jamii mpya inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano.

Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unatekelezwa kwa raia wote pasi na ubaguzi wa kidini au kikabila. Sheria zitoe haki sawa kwa wote, sanjari na uhuru wa dhamiri unaofumbatwa katika uhuru wa kuabudu. Serikali inayotekeleza dhamana na wajibu wake inapaswa kuwahakikishia raia wake wote ustawi na maendeleo endelevu. Kumbe, kuna haja kwa Serikali kushirikiana kikamilifu na viongozi wa dini mbali mbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Viongozi wa kidini kwa upande wao, nao wanapaswa kukemea na kulaani kwa nguvu zote vitendo vya kigaidi, uvunjifu wa haki msingi za binadamu na mauaji ya kimbari kwa misingi ya udini usiokuwa na mashiko wala mvuto! Hakuna dini inayoweza kuhalalisha mauaji kwa jina la Mungu. Kwa bahati mbaya kuna mambo ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni yanayotumiwa na baadhi ya viongozi kuchochea vurugu na mipasuko ya kidini na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Askofu mkuu Gallagher anakaza kusema, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Elimu makini na endelevu, ipewe msukumo wa pekee kwa vijana wa kizazi kipya, ili iweze kuwasaidia kupambana kikamilifu na changamoto za maisha. Vijana wasipoelimishwa vyema kuwajibika katika ustawi, maendeleo na mafungamano ya kijamii, wanaweza kutumiwa na wajanja wachache katika jamii kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Umaskini wa kipato, mmong’onyoko wa kimaadili na kiutu, umepelekea baadhi ya viongozi kutumiwa kuvuruga misingi ya amani na usalama kati ya watu kwa kupandikiza chuki na uhasama kati ya watu. Matokeo yake ni vita na ghasia za kidini zinazotumika kuendeleza biashara haramu ya silaha duniani kama anavyosikitika kusema Baba Mtakatifu Francisko. Kumbe, ulinzi na usalama, haki, amani; maisha, utu na haki msingi za binadamu ni mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuyavalia njuga ili kudumisha haki, uhuru wa kuabudu na kidini kati ya watu wa Jumuiya ya Kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.