2017-09-25 08:48:00

Caritas Africa: Tamko la Dakar, Senegal, 2017


Kanisa katika ulimwengu mamboleo linapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika  matendo ya huruma kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya na wa kina Barani Afrika unaojikita katika huduma makini: kiroho na kimwili kama ushuhuda wa maisha na kielelezo cha imani tendaji. Upendo wa Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba upendo wa kibinadamu unapata utimilifu wake katika upendo wa kimungu unaogusa, unaoganga na kuponya mahangaiko ya binadamu. Kanisa linapenda kukazia huduma ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wake na kwamba, upendo wa Kimungu unalikamilisha na kuliwezesha Kanisa Barani Afrika kusimama kwa miguu yake katika huduma.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa Barani Afrika, Caritas Africa, kuanzia tarehe 18 - 21 Septemba, 2017 imeadhimisha mkutano wake mkuu huko Dakar, Senegal kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kuratibu huduma ya upendo Barani Afrika: Wajibu wa Maaskofu”. Waraka wa “Huduma ya upendo” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na Waraka wa “Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko zimekuwa ni nyaraka elekezi katika mkutano wa Caritas Africa mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Mkutano wa Dakar, umehudhuriwa na Marais kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM pamoja na Wakurugenzi wa Caritas Kitaifa kutoka katika nchi 43 Barani Afrika. Tamko la Dakar linakazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa wafanyakazi wa Caritas Africa kuwa ni kuendelea kutenda kama mashuhuda amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Caritas Africa inamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe aliowatumia washiriki mkutano huu kupitia kwa Askofu mkuu Michael W. Benach, Balozi wa Vatican nchini Senegal, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa kibaba wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa Kanisa Barani Afrika. Mababa wa Afrika wanaishukuru familia ya Mungu nchini Senegal, chini ya uongozi wa Rais Macky Sall kwa ukarimu wake wote.

Tamko hili linabainisha kwamba, Nyaraka mbali mbali zilizotolewa na viongozi wa Kanisa katika miaka ya hivi karibuni zimewawezesha kutambua asili ya Kanisa katika huduma ya upendo kama kiini cha maisha na utume wake kama Jumuiya ya imani na upendo. Wanamshukuru Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu na viongozi wa Shirikisho la Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa mchango wao katika kuwahimiza Mababa wa Kanisa Barani Afrika kuwa ni mashuhuda wa upendo kwa Makanisa mahalia. Wanahamasishwa kuchukua muundo mpya wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu na kuumwilisha katika miundo ya Makanisa mahalia kwa ajili ya utekelezaji wa huduma makini na endelevu kwa watu wa Mungu Barani Afrika.

Caritas Africa inasema, familia ya Mungu Barani Afrika itaendelea kushirikisha imani katika matendo, changamoto inayofanyiwa kazi katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo sanjari na kuendelea kupanua wigo wa ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ndani na nje ya Bara la Afrika. Uzoefu, mang’amuzi na changamoto walizoshirikishana Mababa wa Caritas Africa wakati wa mkutano wao ni kielelezo makini cha Kanisa la Kristo linalojikita katika huduma endelevu ya binadamu, licha ya changamoto zinazoendelea kuibuliwa ambazo zinahitaji mang’amuzi na kipaji cha ubunifu kinachomwilishwa katika utume na shughuli za kichungaji zinazofanywa na Mama Kanisa Barani Afrika.

Caritas Africa inaunga mkono tamko la Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka Colombia kwamba, Bara la Afrika si mahali pa kunyonya, bali rafiki anayepaswa kupendwa na kusaidiwa ili hatimaye, aweze kukua na kukomaa. Caritas Africa inayashukuru Makanisa na wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu ya binadamu, waliowashika mkono katika huduma makini ya binadamu Barani Afrika, hasa miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, mwaliko wa kuwainjilisha hata hawa kwa njia ya huduma makini!

Caritas Africa katika tamko lake la Dakar, Senegal, inaendelea kufafanua kwamba, mapungufu katika utendaji wake wa kazi, kisiwe ni kisingizio cha kubweteka na kuanza kusubiri msaada wa maendeleo endelevu kutoka nje, kwani maendeleo ya kweli yanaweza kupatikana kwa maskini kuunganisha nguvu zao, ili kupambana kikamilifu na changamoto za maisha yao. Kutokana na mantiki hii, Caritas Africa ina thamini sana ushirikiano na mshikamano miongoni mwa Makanisa, kwa kushirikishana mtaji, rasilimali watu na vitu; uzoefu na mang’amuzi katika huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu katika ngazi mbali mbali ni msaada na mwongozo mkubwa wa jitihada za Caritas Africa katika huduma.

Caritas Africa inasikitika kusema kwamba, wakati mwingine, mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu Barani Afrika yanasababishwa na viongozi wa Afrika wanaoshirikiana na mataifa na mashirika ya kigeni katika hujuma ya rasilimali ya Afrika ambayo ingetumika kwa ajili ya kupambana na umaskini. Matokeo yake ni ghasia na machafuko yanayosababisha vijana wengi ambao ni nguvu kazi, kulikimbia Bara la Afrika au kutumiwa katika machafuko ya kisiasa na misimamo mikali ya kidini.

Caritas Africa inamwomba Roho Mtakatifu ili alisaidie Kanisa Barani Afrika kuwa ni mlinzi mwema wa huduma ya upendo. Caritas Africa inataka kujizatiti zaidi kusimama kidete kulinda na kutetea rasilimali ya wananchi kama vile ardhi ili isipokwe na wajanja wachache kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika. Caritas itaendele kutoa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji wahanga wa: vita, ghasia, majanga asilia pamoja na kuendelea kujielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya mambo yote yale yanayosababisha umaskini Barani Afrika, ambalo limebahatika kuwa na rasilimali watu hasa vijana ambao ni nguvu kazi; utajiri wa asili pamoja na mila na tamaduni njema. 

Caritas inasema, inaanza kujiandaa kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 mjini Vatican, ili kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa nyumbani wanapokuwa ndani ya Kanisa. Caritas kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo endelevu ya binadamu, inapenda kuwajengea vijana uwezo kwa njia ya elimu na malezi makini kama sehemu ya ukuaji wa maisha ya kiroho na kama raia wema.

Caritas Africa inataka kujizatiti zaidi katika mchakato wa kuwashirikisha wanawake katika ustawi na maendeleo ya familia na jumuiya zao na kwamba, Caritas inaendelea kuwatia shime viongozi na wasomi wa Bara la Afrika kusimama kidete kupinga rushwa na ufisadi, kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema; ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika badala ya kutawaliwa na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka.

Caritas Africa itaanza kufanya marekebisho ya miundo mbinu yake kwa Makanisa mahalia, ili kwenda sanjari na muundo mpya wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu lililoanzishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko. Caritas Africa, inapania kujifunga kibwebwe katika mchakato wa maboresho ya utawala bora mintarafu huduma za kijamii, kwa kujiwekea sera makini na kuwatumia watu waliobobea katika huduma. Caritas Africa inapania pia kuweka Mafundisho Jamii ya Kanisa; misingi ya ukweli na uwazi katika kuratibu na matumizi ya rasilimali ya Kanisa kwa ajili ya huduma ya maskini kuwa ni sehemu ya malezi Seminarini na kwenye nyumba za kitawa.

Caritas Africa mwishoni, inataka kuratibu kikamilifu huduma yake kwa Bara la Afrika kwa kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Majimbo katika ujumla wake ili kujenga umoja wa Kikanisa na huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu; kuimarisha umoja na mshikamano na wadau mbali mbali wa maendeleo ili kujenga utamaduni wa amani na maendeleo ya kweli yanayofumbatwa katika utambulisho wa Kanisa Katoliki kwamba, huduma ya upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.