2017-09-23 16:43:00

Zingatieni haki msingi, utu na heshima ya binadamu ili kupata amani


Haki msingi, utu na heshima ya wananchi wa Siria vinapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa na wote. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria, uhuru wa kuabudu na usawa wa raia wote wa Siria mbele ya sheria vinadumishwa bila ubaguzi wa aina yoyote ile, mambo msingi yanayoweza kujenga: haki, amani na maridhiano kati ya wananchi ndani na nje ya Siria.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, hivi karibuni, wakati wa kuchangia hoja kwenye mkutano kuhusu hali ya kisiasa nchini Siria ulioandaliwa na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya kwenye Umoja wa Mataifa. Lengo kuu la mkutano huu ni kutafuta suluhu ya muda mrefu itakayosaidia mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mkutano huu umefanyika sanjari na mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huko New York, Marekani.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, amefafanua kwamba, suluhu ya kudumu kisiasa ndani ya Siria ni muhimu sana kuweza kufikia amani ya kudumu kati ya watu wa dini na makabila mbali mbali nchini Siria. Vatican kwa upande wake, itaendelea kujikita katika kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii nchini Siria. Kanisa linaguswa sana na matatizo pamoja na mahangaiko ya wananchi wa Syria, hasa mahangaiko ya watoto na wanawake wanaonyimwa haki zao msingi na huduma makini.

Vatican inawataka wadau mbali mbali wa vita nchini Siria kutoa nafasi ili misaada ya kiutu iweze kuwafikia walengwa na kwamba, sheria na haki ya kimataifa haina budu kuheshimiwa, kwa kuwalinda raia na mali zao pamoja kuheshimu miundo mbinu ya huduma. Mwelekeo huu pia umeungwa mkono na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya chini ya Federica Mogherini na kwamba, Umoja huu uko tayari kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kuhusu Siria kwa Mwaka 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.