2017-09-23 09:54:00

Wema na huruma ya Mungu inawagusa hata wale walioko kijiweni!


Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema. Bwana ni mwema kwa watu wote; na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote; na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao kwa uaminifu! Hii ni sehemu ya wimbo wa kati kati katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Ni maneno ambayo yanatufunulia kwa muhtasari mawazo ya Mungu ambayo ni kinyume kabisa cha mawazo ya binadamu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake hapa duniani, ametufunulia: ukuu  na haki ya Mungu; wema na utakatifu wake, huruma na msamaha kwa wote wanaotubu na kumwongokea katika maisha yao, hata kama watachelewa na kufanya kazi kwa saa moja tu!

Kristo Yesu katika Injili ya leo, aliyafahamu sana mazingira ya kazi wakati wa mavuno ya zabibu. Hii ilikuwa ni kazi iliyohitaji nguvu kazi na mara nyingi, watu walipewa kazi kutokana na sifa njema mbele ya watu, kumbe, wale waliokuwa wanaaangaliwa kwa ”jicho la kengeza” na jamii ilikuwa ni vigumu sana kupata ajira kwa wakati. Kila mtu alipewa ujira wake wa haki kadiri ya muda wa kazi. Lakini, katika Injili ya leo hata wale wa mwisho, waliokuwa wanajikongoja, wamepata ujira sawa na wale walioajiriwa kwanza kabisa! Hapa wale wafanyakazi walioajiriwa kwanza kabisa, wanapinga kwa nguvu zote haki ya mwenye shamba!

Nadhani hapa wengi wetu tungeangukia katika mawazo kama haya ya ubinafsi kwa kuelemewa na falsafa ”Eti, mbuzi hula kadiri ya urefu wa kamba yake”. Mwenyezi Mungu anajibu kwa kusema, ni halali yake kutumia mali yake kwa ajili ya kutenda wema. Yesu anatumia mfano wa maisha ya kawaida ya binadamu na kuyamwilisha kuwa ni kiini cha ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu inayofafanua wema, huruma, ukuu na utakatifu wa Mungu na kwamba, mawazo na njia za binadamu ni tofauti kabisa na mawazo na njia za Mungu anayewalipa wote kadiri ya mapenzi yake kwani Mungu ni mwema.

Hiki ndicho kiini cha Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXV ya Mwaka A wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume” Misericordiae vultus” yaani ”Uso wa huruma” anakaza kusema, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu. Anajisikia kuwajibika, kwani anatamani kuwaona watoto wake wakiwa na afya njema: kiroho na kimwili! Watu wanaosheheni furaha kama mashuhuda na vyombo vya Injili; watu wenye amani na utulivu moyoni! Katika Injili, Mwenyezi Mungu anajitaabisha kwenda kuwatafuta wafanyakazi ”vijiweni” huko ambako wanapiga michapo na kulumbana kuhusiana na masuala ya vyama vyao vya kisiasa! Watu hawa wanabahatika kuajiriwa kwa muda wa saa moja, lakini wote wanapata ujira sawa sawa na wale waliohenyeka siku nzima!

Manung’uniko ya wafanyakazi hawa yanabebwa katika mazoea ya haki na kusahau kwamba, hii ni hatua ya kwanza muhimu, lakini inapaswa kukamilishwa na ushuhuda wa huruma, vinginevyo, Baba Mtakatifu Francisko anasema, maisha yanakuwa ni tasa! Si mali kitu! Ni ubatili mtupu! Wafanyakazi hawa kutoka kijiweni, wameshirikishwa furaha, huruma na msamaha, kama njia ya kubeba mateso na mahangaiko ya watu hawa ambao hawakuwa na fursa ya kazi tangu mwanzo. Huruma ni chachu ya maisha mapya na ujasiri wa kuweza kuyaangalia na kuyaambata yajayo kwa moyo wa shukrani na matumaini thabiti!

Tunakumbushwa kwamba, uvivu ni kichaka cha shetani katika maisha ya binadamu. Kukaa bure kunahatarisha maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Lakini kuna sababu mbali mbali zinazowafanya watu kukosa fursa za ajira, jambo ambalo kwa sasa ni changamoto pevu sana hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Hii inatokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na hali mbaya ya uchumi, kiasi kwamba si rahisi sana kupata ajira.

Mtakatifu Ambrosi anasema, kila mfanyakazi ni mkono wa Kristo ambao unaendelea kuumba na kutenda mema. Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu! Usichezee kazi, chezea mshahara ambao ni haki yako! Utu na heshima ya binadamu vinapaswa kulindwa na kudumishwa mahali pa kazi! Kanisa linafundisha kwamba utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima ya kazi! Kazi ni wajibu! Huu ndio ufunuo wa wema, huruma na upendo wa Mungu kwa maskini anayeguswa na mahangaiko ya watu wake, anayetamani kuwaona wafanyakazi wote wakirejea nyumbani kwa furaha kwa sababu wanao mshahara utakaowawezesha kutekeleza wajibu na dhamana yao ndani ya familia. Ukitaka kujua uchungu wa kukosa kazi, chezea kazi!

Kila mtu awaye yote! Watakatifu na wadhambi, wote wanaitwa na kualikwa kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa ufalme wa Mungu. Mafarisayo waliwabeza sana watoza ushuru na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; lakini hawa ndio waliopata upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Yesu, wakatubu na kumwongokea Mungu, kiasi hata cha kuurithi Ufalme wa Mungu. Yesu ni njia, ukweli na uzima; ni mwanga wa Mataifa. Ikumbukwe kwamba, hii ni sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo, mtoza ushuru, aliyeangaliwa na Yesu kwa jicho la huruma na mapendo, leo hii ni shuhuda wa Injili ya Kristo!

Hii ni changamoto hata kwa waamini wa nyakati hizi, ambao wanadhani kwamba, Kanisa ni kwa ajili ya watakatifu na wanyofu wa moyo peke yao! Lakini, Kanisa ni Jumuiya ya watakatifu na mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake! Ni Jumuiya ya wadhambi wanaojitahidi kutubu na kumwongokea Mungu katika hija ya maisha yao, wengine wameanza safari hii mapema, lakini kuna wale ambao bado watafika saa kumi na moja za jioni! Wote hawa wanataka kuonja: ukuu  na haki ya Mungu; wema na utakatifu wake, huruma na msamaha ili hatimaye, waweze kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Watu hawa wa saa kumi na moja, nao pia wanataka kuwa ni watoto wam wanga, ili waweze kutembea katika mwanga mpya wa Pasaka, kwa kuuvua utu wao wa kale. Upendo kwa Mungu na jirani, iwe ni dira na muhtasari wa maisha na utambulisho wa Wakristo! Tusipokuwa na moyo wa toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika unyenyekevu, tutashindwa kuona wema, huruma, upendo na ukuu wa Mungu katika maisha ya waja wake. Leo hii, tuwe na ujasiri wa kutubu na kumwongokea Mungu; katika shida na mahangaiko ya maisha, tukimbilie katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, kwa kuishi mikononi mwake, ili Kristo aweze kutukuzwa kati ya watu wake! Tuwe na jicho la huruma na mapendo kwa jirani zetu; tutubu na kumwongokea Mungu, ili tuanze maisha mapya katika Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.