2017-09-23 15:48:00

Papa Francisko: Watawa zingatieni: Sala, kiasi na umoja katika upendo


Mama Kanisa anamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumjalia Jumuiya za watawa wa kimonaki wasiokuwa na mbadala katika maisha na utume wa Kanisa; kielelezo cha utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, yanayowachangamotisha waamini kutafuta mambo yaliyo juu na kuishi kadiri ya mpango wa Mungu. Haya ni maisha na utume unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya sala endelevu;  kiasi na umoja katika upendo. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 23 Septemba 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wanaoshiriki katika mkutano mkuu wa Shirika la Watawa wa Cistercians.

Baba Mtakatifu amefafanua kwamba, maisha ya sala endelevu ni ushuhuda wa upendo wao kwa Mungu na binadamu unaodhihirishwa kwa namna ya pekee katika matendo ya Mungu kwa mwanadamu. Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kusoma, kutafakari na kusali Neno la Mungu, chemchemi ya sala na tafakuri. Hii ni dhamana inayowataka kuwa waaminifu na wadumifu, ili hatimaye, waweze kuwa ni watu wa sala wanaokumbatia upendo wa Mungu unaowageuza na kuwafanya kuwa ni marafiki zake.

Watawa wawe ni mabingwa katika maisha ya sala, waaminifu katika maisha yao ya kiroho na kimwili; kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazoratibisha maisha yao ili kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya ushuhuda huu wa maisha, watawa hawa wataweza kuwa kweli waalimu na mashuhuda wanaomwimbia masifu Kristo Yesu; wanaosali na kuombea wokovu wa watu wote. Nyumba za kitawa ziwe ni mhali ambapo watu wanapata amani, utulivu wa ndani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye ndiye peke yake anayeweza kuwakirimia kwani ni kimbilio salama!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa hawa kuwa na kiasi katika maisha yao ili kuweza kutoa kipaumbele cha pekee kwa mambo msingi katika maisha, ili hatimaye kupata furaha ya kukutana na Kristo Yesu. Maisha ya kiasi yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika ushuhuda kwa walimwengu mamboleo ambao wanapenda na kutamani sana anasa katika maisha yao na matokeo yake ni furaha isiyokuwa na mashiko wala mvuto!

Baba Mtakatifu anawasihi watawa kudumisha umoja na mshikamano katika maisha ya kijumuiya; ushuhuda wa upweke binafsi na mshikamano unaowaunganisha wanajumuiya wote katika kifungo cha upendo. Uzoefu na mang’amuzi haya ya maisha ya kiroho yanapaswa kumwilishwa katika maisha ya kijumuiya kwa kuwashirikisha wanajumuiya wenzao katika tafakari ya binafsi, maadhimisho ya liturujia ya Kanisa; ukarimu kwa wale wanaotafuta amani na utulivu wa ndani ili kuweza kutafakari na kujenga uhusiano na Mwenyezi Mungu, kwa kutambua kwamba, Shirika lao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Kanisa. Watawa wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda wa watu wanao mtafuta Mungu, shule ya sala na upendo kwa wote!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Katiba ya upendo ni kiini cha wito na ukweli wa maisha ndani ya Kanisa, changamoto na mwaliko kwa watawa hawa kujenga na kudumisha umoja katika upendo, kielelezo cha familia ya kitawa inayoitwa kumfuasa Kristo Yesu kwa ukaribu zaidi katika maisha ya kijumuiya yanayofumbatwa katika udugu. Umoja katika upendo unashuhudiwa pia katika amana ya maisha ya kiroho, utambulisho makini wa Shirika lao. Maadhimisho ya mkutano mkuu wa Shirika iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano; kujenga utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana kwa makini; umoja katika jitihada za kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha.

Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kujichunguza kuhusu ubora wa ushuhuda wa maisha yao; uaminifu kwa karama na maisha ya jumuiya zao za Kimonaki, daima wakijitahidi kusimama kidete kulinda karama ya Shirika ambayo ni wajibu mkuu wa Mkutano mkuu wa Shirika kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Shirika hili katika hija ya historia ya maisha yake, limeonja mafanikio makubwa na hata wakati mwingine shida na mahangaiko, lakini daima limeendelea kuwa aminifu katika wito wa kumfuasa Kristo Yesu, ili siku moja waweze kufikia utukufu wa Mungu, ustawi na mafao ya watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika watawa hawa kusoma kwa uaminifu historia ya Shirika lao mintarafu mwanga na giza lililowakumba; upya ulioletwa na Roho Mtakatifu na hatimaye, kubainisha kwa ujasiri uwezekano na fursa za ushuhuda wa karama ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ushuhuda na mafungamano miongoni mwa watawa hawa na kwamba, anawaweka wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Anawaomba hata wao kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sala na sadaka zao nyofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.