2017-09-23 16:22:00

Papa Francisko: utekelezaji wa Ijumaa ya huruma ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, alijiwekea utaratibu wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha yake, dhamana ambayo anajitahidi kuiendeleza kila wakati anapopata fursa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ijumaa, tarehe 22 Septemba 2017, Baba Mtakatifu alitembelea Kituo cha Mfuko wa Santa Lucia, mjini Roma. Hiki ni kituo kinachotoa huduma makini kwa walemavu wa viungo pamoja na magonjwa mbali mbali! Hiki ni kituo cha mazoezi ya viungo.

Baba Mtakatifu anaendeleza maadhimisho ya mwaka wa huruma ya Mungu kwa kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wanaoteseka: kiroho na kimwili! Baba Mtakatifu alipowasili katika Kituo hiki alilakiwa na viongozi wakuu wa Mfuko huu pamoja na baadhi ya wafanyakazi, wakiongozwa na Dr. Edoardo Alesse, Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Santa Lucia. Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kutembelea kitengo cha watoto walemavu wanaofanyishwa mazoezi ya viungo kituoni hapo. Amepata nafasi ya kushuhudia baadhi ya watoto hawa wakifanyishwa mazoezi, ili hatimaye, waweze kurejea walau katika hali yao kawaida.

Baba Mtakatifu pia alibahatika kutembelea wodi ya vijana wenye umri kati ya miaka 15- 25. Wengi wao ni wale waliopata ajali barabarani na kwenye viwanja vya michezo. Mwishoni, Baba Mtakatifu alitembelea kitengo cha mazoezi ya wazee na kuwatia shime wote kufanya mazoezi mara kwa mara kwa ajili ya kudumisha afya zao, daima wakitegemea huruma ya Mungu na jitihada za madaktari kutokana na maendeleo ya sayansi na tiba ya mwanadamu! Baba Mtakatifu alihitimisha Ijumaa ya huruma ya Mungu kwa kusali na kutafakari kwa kitambo kidogo kwenye Kikanisa kilichoko kwenye kituo hiki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.