2017-09-23 16:59:00

Makovu ya Tsunami Jimboni Sendai bado yanaonekana sana kwa watu!


Baba Mtakatifu Francisko anawakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu Jimboni Sendai, nchini Japan, waliokumbwa na Tsunami kunako mwaka 2011 na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hata katika mazingira haya ya kukatisha tamaa, bado Mwenyezi Mungu anawakumbuka waja wake. Bado kuna makovu makubwa ya maafa yaliyosababishwa na Tsunami na kwamba, watu kwa ari, moyo mkuu na matumaini, wanaendelea kujenga maeneo yao!

Haya yasemwa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Ijumaa tarehe 22 Septemba 2017 alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Jimbo Katoliki la Sendai, akiwa ameambatana na Askofu Martin Tetsuo Hiraga, Askofu Tarcisius Isao Kikuchi wa Jimbo Katoliki la Niigita pamoja na Askofu mkuu Joseph Chennoth, Balozi wa Vatican nchini Japan. Kardinali Filoni alipata nafasi ya kutembelea na kujionea mwenyewe athari iliyosababishwa na Tsunami kunako mwaka 2011.

Wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Kardinali Filoni alionesha masikitiko yake makubwa kutokana na maafa makubwa yaliyosababishwa na Tsunami kiasi cha kusababisha mabadiliko makubwa katika mtindo wa maisha na utume wa mapadre na watawa katika eneo hili. Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba, Kanisa daima limeendelea kuwa bega kwa bega la familia ya Mungu Jimboni Sendai hata katika shida na mahangaiko yake. Katika mazingira kama haya, waamini wengi hupenda kujiuliza maswali msingi, kwanini kuna kifo na majanga asilia sehemu mbali mbali za dunia, yanayosababisha watu wasiokuwa na hatia kupoteza maisha yao!

Maswali yote haya yanaacha ukakasi katika mawazo na maisha ya watu. Hata katika Maandiko Matakatifu kuna watu waguswa na mateso na mahangaiko katika maisha yao, kiasi hata cha kuhoji uwepo wa Mungu! Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitembea sehemu mbali mbali akitangaza na kuhubiri Habari Njema ya Wokovu, akiponya magonjwa na kuwarejeshea tena watu utu na heshima yao kama wana wapendwa wa Mungu. Hii ndiyo dhamana na utume unaoendelezwa na Mama Kanisa hata kwa watu wa nyakati hizi. Kardinali Filoni anasema uwepo wake kati yao ni alama ya ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hata katika hali kama hii ya kukatisha tamaa, lakini bado Mwenyezi Mungu anapenda kuonesha uwepo wake wa daima. Kanisa zima la kiulimwengu linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa familia ya Mungu Jimboni Sendai na kwamba, kamwe hawawezi kusahaulika!

Na  Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.