2017-09-23 17:13:00

Hija ya Papa Francisko nchini Perù kuimarisha mafungamano ya kijamii


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Septemba 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Pedro Pablo Kucyzynski Godard wa Perù pamoja na ujumbe wake, ambaye baadaye amebahatika pia kukutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambata na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu Msaidizi wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Rais Godard yamefanyika katika hali ya amani na utulivu mkuu, kwa kugusia masuala muhimu ya mahusiano kati ya Vatican na Perù, ambayo yataimarishwa zaidi wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù.

Katika mazungumzo ya viongozi hawa wawili, wamegusia masuala ya vijana wa kizazi kipya mintarafu elimu makini; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; maendeleo endelevu ya binadamu sanjari na mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato. Wamepongeza mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Perù. Mwishoni, wamegusia pia masuala makuu ya kikanda na kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.