2017-09-23 16:07:00

Dumisheni: Ufukara wa Kikristo, Useja na Utii!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumamosi, tarehe 23 Septemba 2017 amekutana na kuzungumza na Majandokasisi wa Jimbo kuu la Tokyo, nchini Japan kwa kukazia umuhimu wa ufuasi wa Kristo Yesu unaofumbatwa katika mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Useja.  Katika mahubiri yake, Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina amefafanua kuhusu mfano wa Mpanzi ambaye ni Mwenyezi Mungu, shamba ni hali na mazingira ya roho za waamini kwani ikiwa kama roho zao zimejiandaa kupokea Neno la Mungu, litaweza kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Kanisa bado lina dhamana na wajibu wa kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo ya Kikristo kama kielelezo makini cha imani tendaji! Majandokasisi kutoka Jimbo kuu la Tokyo, wamekumbushwa kwamba, wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa nchini Japan, kwani Mama Kanisa kwa namna ya pekee kabisa anatumaini ukarimu na sadaka yao kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Tokyo ni Jiji lenye watu na mambo mengi; una fursa na changamoto zake katika maisha, malezi, makuzi na majiundo ya kikasisi. Kuna changamoto zinazokinzana na tunu msingi za Kiinjili, jambo ambalo linawataka Majandokasisi kuwa makini zaidi kwa kujikita katika Mashauri ya Kiinjili yaani; Ufukara wa Kikristo; Useja na Utii.

Ufukara wa Kikristo unaliwezesha Kanisa kumtumikia Mungu na binadamu kwa moyo wa ukarimu na mapendo. Rasilimali mbali mbali ambazo Mama Kanisa amebarikiwa kuwa nazo: kiroho, kimwili, kimaadili na kiutu zinapaswa kutolewa kwa ajili ustawi, maendeleo na ustawi wa watu wa Mungu. Majandokasisi wakijisahau na kumezwa na malimwengu, watazama na kupotelea huko. Useja ni sadaka na majitoleo kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; ushuhuda wa Fumbo la Pasaka unaojikita katika udumifu wa maisha na wito wa kipadre na wala si jambo la mpito!

Majandokasisi wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuondokana na utamaduni wa mambo mpito kwa kukazia mambo msingi katika maisha yao, hata kama yanahitaji sadaka na majitoleo makubwa. Ni wajibu wa Majandokasisi kutoka Japan kushuhudia upendo wa kweli unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia uaminifu na ukarimu! Utii wa Kikristo ni sadaka ya utashi wa mwamini unaotolewa kwa ajili ya Mungu kama Kristo Yesu alivyoonesha utii kwa Baba yake wa mbinguni kiasi hata cha kufa juu ya Msalaba ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Mapadre wanapaswa kujisadaka na kujimega bila ya kujibakiza kama mkate safi unaotolewa kwa ajili ya utukufu wa Mungu na utakatifu wa maisha ya watu wa Mungu! Haitoshi kuwa Padre, bali Kanisa linawahitaji: Mapadre: wema, watakatifu na wachapakazi; watu ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya Mungu, Kristo, Kanisa na Jirani zao. Uhuru wao wautumie kikamilufu katika kuteleleza mapenzi ya Mungu. Alama hizi tatu ni ushuhuda wa kinabii unaowaunganisha waamini katika Fumbo la Msalaba wa Kristo, tayari kujisadaka ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Majandokasisi ni ushuhuda wa matumaini ya Mungu kwa Kanisa nchini Japan, kumbe, wanapaswa kuwa na ujasiri na kwamba, Mwenyezi Mungu atawakirimia neema na baraka wanazohitaji katika maisha na utume wao. Daima wamwangalie Kristo Yesu, ikiwa kama wanataka kudumu katika safari ya wito na maisha yao kama Mapadre wa baadaye!

Kardinali Filoni katika mahubiri ambayo hivi karibuni yalichambuliwa vyema na Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana anasema, kila mwamini anapaswa kutengeneza mazingira yatakayoliwezesha Neno la Mungu kuota, kukua na kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Daraja Takatifu ni zawadi kutoka kwa Mungu inayohitaji mazingira yatakayoiwezesha kukua na kukomaa kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, ni mpole na mkarimu, changamoto kwa waamini ni kujenga utamaduni wa kumsikiliza kwa dhati.

Kanisa la Mungu nchini Japan bado linawahitaji watenda kazi katika shamba la Bwana; wafanyakazi waaminifu, wakweli, watu wenye ibada na wachamungu, watakaoshiriki katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, ushuhuda wa upendo wa Kristo na Kanisa lake, unapenya akili na nyoyo za watu wa Japan. Watu wana kiu ya Neno la Mungu katika maisha yao. Kardinali Fernando Filoni anawaalika Majandokasisi kumwendea Bikira Maria ili aweze kuwafunda katika shule yake, ili kujifunza ujumbe na mtindo wa maisha kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.