2017-09-22 16:05:00

Wayesuit na Vatican watiliana sahihi mkataba wa huduma ya mawasiliano


Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican, kwa niaba ya Sekretarieti hii na Padre Juan Antonio Guerrero Alves kwa niaba ya Shirika la Wayesuit, Alhamisi, tarehe 21 Septemba 2017 wametiliana sahihi kwenye mkataba wa ushirikiano wa Wayesuit katika tasnia ya mawasiliano ya jamii inayosimamiwa na kuongozwa na Vatican, mintarafu mchakato wa mageuzi yanayoendelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu.

Monsinyo Dario Edoardo Viganò amewashukuru na kuwapongeza Wayesuit kwa huduma na mchango wao mkubwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii. Tukio hili linalofungua ukurasa mpya kwa maisha na utume wa Wayesuit, limetiwa mkwaju, siku chache tu baada ya Padre Antonio Stefanizzi, Myesuit, aliyewahi kuwa Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican, tarehe 18 Septemba 2017 kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa, yaani tarehe 18 Septemba 1917 huko Lece, Kusini mwa Italia.

Padre  Stefanizzi ni kiongozi aliyetekeleza dhamana na wajibu wake wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kutilia mkazo walengwa wakuu wa mawasiliano ya jamii. Alifanikiwa kuwapatia watu wa Mungu, ujumbe wa matukio makuu yaliyokuwa yanajiri wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto ambayo imefanyiwa kazi pia na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko kwa wakati huu.

Monsinyo Viganò ametoa shukrani zake za dhati kwa Shirika la Wayesuit, lakini kwa namna ya pekee Wayesuit wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii yanayoratibiwa na Vatican. Mkataba huu ni mwendelezo wa huduma ya mawasiliano yanayotolewa na Wayesuit katika mawasiliano ya jamii katika mapana yake. Anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaridhishwa pia na mtindo mpya wa ushirikiano katika tasnia ya mawasiliano kama sehemu ya mchakato wa mageuzi yanayotekelezwa na Baba Mtakatifu.

Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican inatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Ushirikiano huu utaliwezesha Kanisa kuendelea kuzama zaidi katika huduma ya mawasiliano kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa badala ya kuwa ni faraja ya mtu binafsi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, taaluma na weledi wa mawasiliano unatumika kadiri ya mpango wa Mungu. Wataalam waliobobea katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wanaweza kutumia karama na weledi wao kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Padre Juan Antonio Guerrero Alves anakaza kusema, mambo yanaendelea kubadilika, kumbe, kuna haja ya kusoma alama za nyakati. Lengo la Wayesuit ni kulihudumia Kanisa la Kristo, kadiri ya mahitaji ya nyakati. Huduma yao katika sekta ya mawasiliano ya jamii inawafanya kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa Kristo na Kanisa lake. Ni matumaini ya Wayesuit kwamba, wataendelea pia kuchangia katika mchakato wa mageuzi yanayotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.