2017-09-22 15:40:00

Vatican yatia sahihi Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Silaha za Nyuklia


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, tarehe 20 Septemba 2017 ametia sahihi kwenye mkataba wa Umoja wa Mataifa unaopiga rufuku silaha za kinyuklia, huko New York, Marekani. Hii ni itifaki iliyopitishwa kunako tarehe 7 Julai 2017, baada ya Umoja wa Mataifa kuanzisha chombo cha kisheria kitakacho dhibiti utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za kinyuklia. Sherehe hii imeadhimishwa wakati ambapo Baraza kuu la Umoja wa Mataifa linaendelea na mkutano wake. Mkataba huu utaanza kutumika rasmi baada ya siku 90 kadiri ya Itifaki ya Mkataba huu, Sheria namba 1.

Askofu mkuu Gallagher anasema, Vatican imeridhia mkataba huu ili kuendeleza mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa maisha unaofumbatwa katika: Uhai, utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni mkataba unaopania kukuza na kudumisha ushirikiano unaowajibisha; majadiliano katika ukweli na uwazi; uaminifu na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Vatican katika masuala ya ushirikiano wa kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wakati wa maadhimisho haya amewataka wajumbe kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kutekeleza yaliyomo kwenye mkataba huu, ili dunia iweze kuondokana na hofu pamoja na wasiwasi wa mashambulizi ya silaha ya kinyuklia. Hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kuhakikisha kwamba, inaunda mazingira yenye ulinzi na usalama pasi na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia. Huu ni wakati wa kutafakari kwa kina na mapana kanuni maadili ya amani, ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa, ili kuondokana na woga pamoja na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko!

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kuheshimiana, kuthaminiana na kuaminiana katika maamuzi na utekelezaji wa vipaumbele vinavyotolewa na Jumuiya ya Kimataifa. Majadililiano katika ukweli na uwazi ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha maendeleo endelevu ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kanuni maadili ya amani, usalama na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa yataendelezwa Zaidi  kwa kuondokana na falsafa ya kuwatenga watu kutokana na misimamo na mitazamo yao katika masuala ya kimataifa.

Mkataba huu wa kimataifa unapiga rufuku: Utengenezaji, majarabio, umiliki na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia. Unakataza kupokea, kutumia na kutolea maelezo matumizi yake. Kila nchi na Serikali inapaswa kutoa tamko lake mbele ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa. Mkataba unatoa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo makini ya amani, madhara ya vita kwa sasa na kwa siku za usoni na kwamba, tasnia ya mawasiliano ya jamii inapaswa kusaidia mchakato wa uragibishaji wa mkataba huu kwa ajili ya ujenzi wa kanuni maadili ya amani, kwani madhara ya mashambulizi ya silaha ya kinyuklia yanaweza kuwa makubwa mno kiasi cha kuwashangaza walimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, matumizi makubwa kwa ajili ya utengenezaji wa silaha za kinyuklia ni kupora rasilimali fedha na nguvu kazi ambayo ingeweza kuwekezwa katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, maboresho ya sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii sanjari na mapambano dhidi ya umaskini wa kutupwa! Ikumbukwe kwamba, waathirika wakuu wa matumizi mabaya ya rasilimali fedha na watu ni maskini ni “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”! Lengo kuu ni kudumisha amani na usalama kati ya watu wa Mataifa sanjari na kujikita katika ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.