2017-09-22 17:17:00

Shirikishaneni ukarimu wa Mungu na jirani; acheni roho ya korosho!


Umimi au ubinafsi ni ugonjwa ambao unaisumbua sana jamii ya leo ya mwanadamu. Kila mmoja anafanya juhudi katika kazi yake ili kuhakikisha anapata zaidi ya mwingine. Mbaya zaidi ugonjwa huu hutujengea chuki kiasi cha kutofurahi kumwona mwingine anapata. Nimejizungushia uzio ambao tunaishi ndani mwake ni mimi mwenyewe na natamani vyote vilivyopo nje vije ndani yangu. Tupo katika jamii ambayo hakuna anayesikiliza kilio cha Lazaro anayeteseka pembeni yangu. Tupo katika jamii ambayo tunahalalisha kuwa aliyepata kapata kwa sababu ya juhudi zake na ataendelea kupata zaidi na aliyekosa amekosa na ataendelea kusota katika kukosa kwake kwani yote ni uzembe wake. Kwa neno moja ni jamii ambayo imeupiga teke upendo wa Mungu, upendo ambao unaufunua ukarimu wake.

Neno la Mungu katika Dominika hii linanuia kututoa katika hali hiyo na kutukumbusha haiba yetu ya kikristo. Ukristo wetu umetuvisha Kristo na hivyo tunapaswa kuuonesha wakati wowote. Mungu anajionesha kupitia kinywa cha Nabii Isaya kwamba anapatikana wakati wowote, na yupo hivyo hivyo katika upendo wake wakati wowote. Nabii Isaya anatuambia: “Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana, mwiteni maadamu yu karibu”. Ni mwaliko wa kuuendea upendo wake kwani Mzaburi ametuambia pia “Bwana yu karibu kwa wote wamwitao”. Hii ndiyo hatua muhimu ya kupiga katika safari ya kiroho, yaani kuutambua uwepo wa Mungu katika maisha yako na kumuita daima. Yeye yupo pamoja nasi na anatusikiliza. Mungu anapatikana wakati wowote tumfungulie mlango. Tumtafute na tusikate tamaa na pia tuwafungulie wenzetu milango ili wamwone Mungu katika ukarimu wake.

Mfano wa Injili unaufafanua udaima huo wa ukarimu wa Mungu. Yeye anaonesha kuwa hakuna kuchelewa katika himaya yake. Yeyote anayemtafuta atampata wakati wowote na haja ya moyo wake itatimizwa. Uwe umeitwa kwake saa tatu au saa kumi na moja wote kwa Mungu ni wenye thamani. Hii inatuonesha kuwa Upendo wa Mungu unajishughulisha daima kutafuta wanaouhitaji. Hata kama sisi tunaukataa au hatujisumbui kuutafuta Yeye anaangaza daima kuangalia haja ya mioyo yetu na kutupatia ukarimu wake mithili ya Baba Mwenye huruma kwa Mwana mpotevu ambaye alimwona mwanaye kwa mbali akirudi, akiitafuta huruma yake na ukarimu wake lakini yeye ndiye akatoka na kumlaki na kumkumbatia kwa upendo mkubwa ( Rej. Lk 15:20).

Nabii Isaya anaendelea kututia moyo kwamba tusikate tamaa na tumtafute Mungu. Tumwendee daima na mioyo ya Toba. “Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asie haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana naye atamrehemu”. Wakati mwingine tunasongwa sana na mzigo wa dhambi na kufikiri kwamba kwa Mungu hakuna tena msamaha, hakuna tena fursa ya kurudi kwake. Bwana anatuambia “mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zangu si njia zenu”. Tumeona Dominika iliyopita akionesha ukubwa wa huruma yake bila kuangalia kiasi au idadi ya makosa. Hii inajidhihirisha pia katika somo la Injili na inautofautisha ukarimu wake huo na mawazo ya kibinadamu. Tunawaona wale waliofika mapema wanapopima kibinadamu na kutaka kuuwekea mipaka ukarimu wa aliyewaajiri. Pamoja na kwamba walipewa ujira wao kadiri ya makubaliano bado walitamani wenzao waendelee kusota kwa malipo duni.

Mungu anapatikana kwa ajili ya wote tuwafungulie mlango. Tunaalikwa kutokuridhika katika kupata wewe tu na pia kutowafungia wengine milango. Tusipime kwa kuangalia yule kapata nini na kwa nini zaidi au pungufu yangu bali tuangalie kwamba yule kapata kilicho cha muhimu katika kujikimu kwa maisha. Ukweli wa kimaisha katika jamii ya leo ya kibepari imejikita katika falsafa ya “survival for the fittest”. Hii tunaweza kuifananisha na msemo unaosema «mbuzi atakula kutokana na urefu wa kamba yake». Katika hii tunahalalisha jamii ambayo inaweka mwanya mkubwa kati ya walio nacho na wasio nacho. Wakati mwingine tunawanyooshea vidole hao wenye kamba fupi wakati sisi ndiyo tuliupunguza urefu wa kamba zao. Yanakuwa ni maisha ya sandakarawe kwamba «mwenye kupata apate na mwenye kukosa akose».

Haina hii ya maisha inapingana na ukristo wetu. Maisha ya kikristo yaufunua ufalme wa Mungu wakati wowote na kwa wote. Waliofika saa tatu katika ufalme hawatofautishwi na waliofika saa kumi na moja. Tungo moja ya nyimbo za dini inasema “Mungu alivyo ndivyo hivyo alivyo: mchana ni yule yule, usiku ni yule yule. Sisi wanadamu ndiyo tunaobadilika na kutoa au kupima kwa kulinganisha. Baba Mtakatifu anatuonya katika hili anapotuambia: “Tunaweza vipi kuhalalisha kwamba tukio la wazee walioachwa katika hali duni kufa si habari nzito lakini nukta moja la soko la hisa inaposhuka inakuwa ni habari kuu? Huu ni unyanyapaa. Tunaweza kundelea kuvumilia kuona chakula kinatupwa wakati watu wengine wanakufa kwa njaa? Huku ni kutokuwa na usawa kati wa wanadamu. Leo hii kila kitu kipo katika mashindano, mwenye nguvu mpishe na hivyo wenye nguvu hufaidi katika walio dhaifu” (Furaha ya Injili n.55).

Ukarimu wa Mungu unaangalia mahitaji na kuinua hadhi. Yeye humgawia kila mmoja ili kuhifahi hadhi yake. Lakini katika ulimwengu wetu wa «mwenye kupata apate» wewe utagawiwa kadiri ulivyochangia. Mwingine hakujali hata kama anayo ya ziada. Ni bora itupwe au ihifadhiwe tu lakini si kukupatia wewe mwingine. Mimi nimeingia saa tatu na wewe saa kumi na moja. Kila mbuzi ale kadiri ya urefu wa kamba yake. Katika mazingira ya kiyahudi ujira wa dinari moja ulikadiriwa kutosha kwa mtu kujikimu kwa siku moja na kuyapata yote muhimu. Wote waliajiriwa saa tatu hata wale wa saa kumi na moja walikuwa na mahitaji hayo ya kawaida ya kibinadamu. Tajiri wa mfano akitufunulia sura ya Mungu mkarimu analitambua hitaji hilo la kila mmoja na anampa kila mmoja kusudi apate haja muhimu za kila siku.

Sehemu ya Neno la Mungu inayotangulia sehemu hii tuliyoisikia leo inatuonesha kitu cha kwanza na cha muhimu ambacho Mungu hutukirimia. Ukarimu wa Mungu unatupatia kwa nafasi ya kwanza uwepo wake, yaani mambo yote mema yanayotoka kwake na si katika mali za kushikika au madaraka ya kidunia. Kristo anawaambia Mitume kuwa kwa Mungu watapata vyote wanavyoacha na ziada. Ni mwaliko unaotutoa katika kung’ang’ana na mambo haya ya kidunia ambayo yanatutenga na ndugu zetu. Leo hii jamii imejaa chuki, kunyonyana na kuibiana ni kwa sababu ya uchu wa mali, umaarufu na madaraka ya kidunia. Mwenyezi Mungu anataka kuwapatia hawa pia uwepo wake yaani ukarimu na upendo wake. Watu wanaohangaika kumtafuta Mungu watauonja huo ukarimu wake kupitia mimi na wewe kwani kanuni ya upendo wa kimungu ni kusambaa kwa wote.

Kuishi katika Kristo kunatupeleka katika kujifunua kwa ajili ya wengine na hata kujimega kwa ajili yao. Mtume Paulo anaonesha kuwa yupo tayari kuitoa nafsi yake kwa ajili ya Kristo ili kuueneza ukarimu wake kwetu. Maisha yake yote yamejaa ukarimu huo na kwa kuwa Kristo ni kiini cha maisha basi anawaunganisha wote na kuwa mfano wa maisha ya kindugu. Tuidhihirishe haiba hiyo tunayoipokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Tuonyeshe shukrani zetu kwa ukarimu wa Mungu kwa sisi nasi kuwa kielelezo cha ukarimu wake kwa wengine. Hii itadhihirisha kwamba kweli Mungu yupo karibu kwa kila anayemuomba kwani ndugu zetu wahitaji tunakaa nao karibu na watakirimiwa na sisi kwa niaba ya Mungu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.