2017-09-22 15:03:00

Papa Francisko: Kanisa litaendelea kutekeleza utume wake kwa maskini


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 22 Septemba 2017 amekutana, amezungumza na kuwapongeza wakurugenzi wa idara ya wahamiaji na wakimbizi kitaifa, wanaoshiriki katika mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, kwa huduma makini wanayoitoa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaobisha hodi katika malango ya Bara la Ulaya ili kupata hifadhi, usalama na maisha bora zaidi! Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji limekuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Ulaya, inayopaswa kuhakikisha kwamba, inatekeleza kwa dhati itifaki ya ulinzi na usalama kama ilivyobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Mama Kanisa anapenda kubaki mwaminifu kwa utume wake wa kumpenda, kumtukuza na kumwabudu Kristo Yesu, hasa miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kati yao ni wakimbizi na wahamiaji. Ushuhuda wa upendo wa Mama Kanisa unapaswa kutolewa kwa watu hawa tangu pale wanapoanzisha mchakato kuzihama nchi zao, wanakopatiwa hifadhi, hadi siku ile mambo yatakapo kamilika na hatimaye, kurejea tena katika nchi zao za asili. Kuna haja kwa Mama Kanisa kuwatambua na kuwasaidia watu hawa ambao wako safarini kama sehemu ya huduma endelevu, inayoratibiwa na yenye tija na ufanisi mkuu.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika sana kuona tabia za ukosefu wa maridhiano, ubaguzi na hofu zisizokuwa na msingi wanazokumbana nazo wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya. Wageni wamekuwa wakiteseka kutokana na ubaguzi unaofanywa dhidi yao na kwa bahati mbaya, kuna hata Jumuiya za Kikanisa zinazohusika na tabia hii inayosikitisha sana, kwa kisingizio cha kutaka kulinda na kuendeleza utambulisho asili wa kitamaduni na kidini. Lakini, ikumbukwe kwamba, Kanisa limekuwa na kupanuka kutokana na hamasa ya wahamiaji wa kimisionari, waliosukumwa kutoka kifua mbele, ili kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.

Hata ndani ya Kanisa, Baba Mtakatifu anasema, daima kumekuwepo na kishawishi cha utengano na ubaguzi wa kitamaduni, lakini Roho Mtakatifu amelisaidia Kanisa daima kuwa wazi na kuwapokea wengine kama chachu ya kukua na kukomaa. Hata leo hii, Roho Mtakatifu anawachangamotisha waamini kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji. Hili ni tukio la pekee kwa wakati huu hasa kutokana na mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa, kiasi cha kuchangia mawazo ya kudhibiti idadi ya nchi wanachama wanaotaka kujiunga na Jumuiya ya Ulaya. Changamoto hii inaweza kutekelezwa kwa makini kwa kuzungatia haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kudumisha umoja na udugu unaobubujika kutoka katika imani kwa Kristo na Kanisa lake; imani ambayo waamini wanathubutu kuiungama kila Jumapili wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Wakimbizi na wahamiaji ni utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kiliturujia na hata katika maisha na utume wa Kanisa Barani Ulaya. Huu ni mwelekeo mpya wa ari na mwamko wa kimisionari, changamoto na mwaliko wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo bila ya kulazimika kutoka katika maeneo ya watu husika. Kinachotakiwa hapa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko; imani inayofumbatwa katika upendo mkamilifu; kwa kuheshimu na kuthamini hata dini za watu wengine; ili kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa sera za mikakati ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia: ukarimu, ulinzi, uhamasishaji na ushirikishwaji; mambo yanayofumbatwa katika sheria, taratibu, kanuni na usalama kwa wakimbizi ili kupata hifadhi na huduma msingi. Ulinzi unafumbata haki msingi za binadamu; uhamasishaji unazingatia ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu na hatimaye ushirikishwaji ni dhana inayoheshimu mwingiliano wa tamaduni za watu, ili kutajirishana katika maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu, hadi kufikia mwishoni mwa Mwaka 2018, katika Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi kutatolewa Mwongozo wa huduma za kichungaji kwa wahamiaji, utakaotumika kwenye Makanisa mahalia; ili kukuza na kudumisha majadiliano na serikali husika kwa kuzingatia Itifaki za Kimataifa. Maneno makuu yaliyotumiwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018 yanaweza kuwa ni dira na mwongozo wa shughuli za kichungaji kwa Makanisa mahalia. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wajumbe hawa kwamba, wao ni sauti ya kinabii inayopaswa kufumbatwa katika Mafundisho tanzu ya Kikristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.