2017-09-22 15:21:00

Papa Francisko: hakuna tena uvumilivu kwa watakaokumbwa na kashfa


Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni jambo ambalo Kanisa kamwe halitaweza tena kulivumilia na kwamba, wahusika watashughulikiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria zilizopo. Nyanyaso za kijinsia ni hatari kwa utu wa binadamu na ukomavu wa watoto wadogo ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kanisa linatambua kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, imekuwa ni kashfa iliyolichafua Kanisa kwani imewaanika hadharani watu waliotumia vibaya wito na dhamana waliyokabidhiwa kwa ajili ya watoto wa Mungu. Hii ni aibu kubwa kwa wakleri, ambao kimsingi wamesaliti imani ya watu wa Mungu kwa kuelemewa na udhaifu wao wa kibinadamu.

Hii ni hotuba kali, iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 22 Septemba 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Baba Mtakatifu anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni dhambi inayotisha na kwenda kinyume kabisa cha mafundisho ya Kristo Yesu. Kumbe, Kanisa katika ngazi zote linapaswa kuwa makini na kuwashughulikia wote watakaokamatwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo bila kukwepesha maneno!

Sheria zilizopitishwa zinawahusu wale wote wanaofanya kazi ndani ya Kanisa na taasisi zake zote. Lakini, Maaskofu, Mapadre na Watawa anasema Baba Mtakatifu Francisko wanayo dhamana na wajibu wa kwanza kabisa katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya watoto wanaokabidhiwa kwao kwa ajili ya malezi na makuzi! Hawa ni watu ambao wameitwa na kupewa dhamana ya huduma kwa ajili ya familia ya Mungu, ikiwa ni pamoja na kulinda na kutetea utu na heshima yao kama binadamu. Baba Mtakatifu amepata pia nafasi ya kukutana na kuzungumza na baadhi ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia. Amewashukuru wajumbe kwa kazi kubwa wanayoendelea kuitekeleza kwa ajili ya kulinda na kudumisha utu na heshima ya watoto.

Baba Mtakatifu anasema umefika wakati wa kusimamia ukweli kwa Kanisa kujielekeza zaidi katika kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zinazo chafua maisha na utume wa Kanisa. Mkutano wa Tume hii ya Kipapa imekuwa pia ni nafasi ya kuweza kushirikishana: uzoefu, mang’amuzi na mbinu mkakati wa kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Ni fursa pia ya kushirikishana kidugu rasilimali watu, vitu na fedha ili kuimarisha mchakato wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza wajumbe wa Tume hii kushirikiana kwa karibu zaidi na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, ili kweli sheria, kanuni, miongozo, sera na mikakati ya Tume hii iweze kumwilishwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia! Anakazia umuhimu wa malezi na majiundo awali na endelevu kwa majandokasisi, wakleri na watawa kwa ajili ya Makanisa mahalia, Mabaraza ya Kipapa; semina kwa Maaskofu wapya pamoja na kuandaa makongamano na mikutano ya kimataifa, ili kufanya upembuzi yakinifu na hatimaye, kuwawezesha watu mbali mbali kufahamu madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Lengo kuu ni kulinda na kudumisha utu na heshima yao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linapaswa kuwa ni mahali pa huruma, msamaha na mapendo hasa kwa wale wote ambao wameteseka na kunyanyasika. Kanisa Katoliki litaendelea kuwa ni hospitali kwenye uwanja wa mapambano, ili kuwasindikiza watoto wake wote katika safari yao ya maisha ya kiroho. Ni mahali pa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana; kushirikishana na kumegeana mbinu mkakati wa mapambano ya maisha ya kiroho; mahali pa kukuza, kuimarisha na kumwilisha imani katika matendo kama kielelezo cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.