2017-09-22 14:59:00

Mkutano wa Kimataifa kuhusu Hadhi ya Mtoto katika Dunia ya Digital 3-6Okt


Kuanzia tarehe 3-6 Octoba 2017 utafanyika Mkutano wa Kimataifa kuhusu “Hadhi ya mtoto katika dunia ya digital, ulioandaliwa na Kituo cha Ulinzi wa Watoto katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani Roma. Watoto na vijana wanaunda robo ya bilioni 3.2 ya watumiaji wa internet duniani. Kizazi hiki cha vijana ni zaidi ya milioni 800 ambao wanaonekana kuwa hatari ya kuwathirika na matumizi mabaya, pia kuwa chanzo cha mambo ya hovyo na yasiyo ya maadili,  kushuka kwa maadili na unyanyasaji wa kijinsia kwenye huduma ya mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Katika kuhamasisha kupambana na hali hii, nguvu ya pamoja ya kijami na taifa inahitaji ili kutafuta ufumbuzi  wa kimataifa. Ni lazima kufanya majadiliano ya wazi na kina kwa pamoja ili kujenga ufahamu zaidi na kuhamasisha vitendo vya ulinzi wa watoto katika mitandao wa moja kwa moja. Aidha taarifa inasema,Mkutano kuhusu  “Hadhi ya mtoto katika Dunia ya digital” ni mkutano wa Kimataifa wa kwanza wa aina yake ambao utawakusanya wadau na viongozi mbalimbali wa kimataifa kutoka katika sekta husika. Na Kituo hiki cha Ulinzi wa watoto katika Chuo Kikuu cha Gregoriani Roma kinawakilisha jiwe la msingi na  thamani kubwa  katika hatua ya mapambano ya Kimataifa dhidi ya  unyanyasaji wa watoto kijinsia  katika mazingira ya digital.

Taarifa ineleza kuwa, Mkutano huo unaweza kushiriki wote lakini kwa mwaliko tu, kwa njia hiyo watashiriki wataalamu wa kitaaluma husika katika mambo ya kidigital, viongozi  wa kisiasa, wawakilishi wa kidini kutoka duniani kote. Hii ni fursa ya kihistoria ili kuweza kukabiliana na ajenda ya sasa katika kupambana na unyanyasaji wa kijinsia wa watoto kwenye mtandao na ulinzi wa watoto katika ulimwengu wa digital. Hiyo pia ni kuheshimu haki za binadamu na hasa kwa watoto wanaoathirika katika dunia hii.

Hatua hiyo ni pamoja na hatua nyingine katika ulimwengu huu ambapo hata mashirika mengi  ya watetezi wa haki za binadamu hasa zile zinazohusu makundi maalumu ikiwemo watoto na wanawake  wamekuwa wakilaani vikali matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ikiwemo vitendo vya watu kusambaza picha za watu waliofanyiwa ukatili au waliopata ajali zikionesha majereha hata maiti zao, badala ya kuokoa uhai wa majeruhi lakini pia hata mauaji ya kinyama yanapotokea picha zimekuwa zikitumwa ovyo bila kujali mahusiano ya mtu atakayeipokea. Ni lazima  mataifa yote kusimamia sheria ya mtandao ili kutunza utu wa mtu lakini pia hata jamii kuacha kuendelea kuwavunjia haki makundi hayo ambayo tayari haki zao zimevunjwa kwani kufanya hivyo ni kunawaathiri na kuchochea maumivu ya kihisia kwake na familia.

Naye Mkuu wa Chuo cha Kipapa cha Gregoriani akielezea zaidi juu ya tukio hilo la Mkutano wa kimataifa, ni heshima kubwa kukaribisha Mkutano Mkuu wa Kimataifa juu ya hadhi ya mtoto katika dunia ya digital. Mkutano Mkuu huo ni mwendelezo wa shughuli za Chuo Kikuu ambao umejikita tangu ifanyike kwa mra ya kwanza Jukwaa kuhusu unyanyasaji wa kijinsia kuelekea uponyaji na kuimarisha uliofanyika mwaka 2012. Mkutano huo umeleta uzinduzi wa Kituo cha Ulinzi wa Watoto wa Taasisi ya Saikolojia ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriana. Ni hatua inayoendelea kujishughulisha na  kile ambacho Baba Mtakatifu mstaafu  Benedikto XVI alikiita kuwa ni  "jeraha wazi la ukiukwaji”.

Na Papa Francisko  alitoa wito kwa upya kuwa na  ujasiri unaojikita katika mienendo inayoweza kutambua ukweli jinsi watoto wetu wengi wanaishi leo hii na kuhakikisha kuwa kwamba heshima ya watoto siyo tu kuheshimiwa lakini zaidi inahitajika  ulinzi. Na ndiyo uwepo wa sasa wa watoto wetu katika ulimwengu wa digital. Vijana huishi na faida, changamoto na vitisho ambavyo zama za digital zinahusisha  kila nchi ya  ulimwengu huu.Hakuna nchi, hakuna taasisi, hakuna mwanadamu mmoja anayeweza kutatua tatizo hili peke yake. Tunapaswa kuungana kwa pamoja katika jitihada hizi za kidini nyingi za kitaifa ili kulinda heshima ya watoto;na  tunapaswa kuelewa kwamba sisi sote tunawajibika  kila mmoja juu ya mwingine duniani.
Anamalizia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Gregoriani Roma akinukuu tena maneno ya Papa  Francisko ya kuwakaribisha wote na kuwatakia mafanikio mema katika kazi yao wakitatafuta ufahamu na ufumbuzi wa masuala ya Mkutano huo katika kukabiliana na kujenga ushirikiamo halisi.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.