2017-09-22 16:52:00

Balozi Petras Zapolskas awasilisha hati za utambulisho


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 21 Septemba 2017 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Bwana Petras Zapolskas, Balozi mpya wa Lithuania mjini Vatican. Alizaliwa kunako tarehe 30 Januari 1965 huko Molètai. Ameoa na amebahatika kupata mtoto mmoja. Katika maisha yake amebahatika kusomea masuala ya uhusiano wa kimataifa na diplomasia katika Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza na kufanikiwa kuhitimu masmo yake kunako mwak 1993. Akajiendeleza kwenye mambo ya ulinzi na usalama huko Marekani na Uerumani hadi mwaka 1995.

Ni mtaalam aliyebobea katika masuala ya uhusiano wa kimataifa na kwamba, amewahi kushika nyadhifa mbali mbali ndani na nje ya Lithuania kama: Mkurugenzi wa masuala ya kisiasa, mshauri na waziri mshauri nchini Russia, Balozi wa muda, Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Balozi nchini Sweden, Mkurugenzi mkuu wa Idara ya Ajira. Kati ya Mwaka 2006 hadi mwaka 2009 alikuwa ni Balozi wa Lithuania, Italia na San Marino; Malta na Libya; Mwakilishi wa Kudumu wa Lithuania FAO na hatimaye, mkurugenzi mkuu wa Idara Itifaki na Diplomasia tangu mwaka 2014 hadi alipoteuliwa kuwa Balozi wa Lithuania mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.