2017-09-21 16:42:00

Vatican yasikitishwa sana na machafuko ya kisiasa huko Afrika ya Kati


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, akishiriki katika mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, hapo tarehe 19 Septemba 2017, ameonesha masikitiko makubwa ya Vatican mintarafu vita, ghasia na mipasuko ya kijamii na kisiasa inayoendelea katika Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Kuibuka tena kwa vita kumepelekea: vifo, ongezeko la majeruhi, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi yao wenyewe.

Vatican inaupongeza mchango mkubwa unaotolewa na Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati, MINUSCA kwa kazi nzuri  inayopania kurejesha tena amani, kuwapokonya silaha wana mgambo wanaoendelea kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo nchini humo! Kuna haja kwa Umoja wa Mataifa kusimama kidete kulinda na kutetea raia pasi na ubaguzi wa aina yoyote ile, ili kuwajengea wananchi moyo wa matumaini na ushirikiano na vikosi hivi vya Umoja wa Mataifa, ili hatimaye, amani ya kweli iweze kurejea tena kwenye Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati.

Kipaumbele cha kwanza lazima kiwe ni ulinzi na usalama wa raia na mali zao sanjari na kurejesha tena amani. Ikumbukwe kwamba, waathirika wakuu ni wanawake na watoto. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati inalindwa na kudumishwa na wote pamoja na kuwahakikishia uhuru wa kutembea, ili kwamba, utu na heshima yao kama binadamu haukumbani na nyanyaso za aina yoyote ile.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake mjini Bangui alikazia umuhimu wa familia ya Mungu nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, kujikita katika tunu msingi za maadili zinazofumbatwa katika uaminifu, utii wa sheria, sadaka na majitoleo ya watu pamoja na heshima; mambo msingi yanayowawezesha watu kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu! Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu mkuu wa kusaidia mchakato wa kurejesha tena demokrasia, maendeleo endelevu na shirikishi kwa watu wote pasi na ubaguzi; utawala wa sheria dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa kikamilifu na Serikali iliyoko madarakani; kwa kutoa huduma bora ya elimu na afya kwa wote.

Changamoto hii anasema Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, inahitaji kwa namna ya pekee kabisa, ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kupata rasilimali fedha na msaada kama sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Mkutano wa Brussels hivi karibuni, ili kusaidia kuwekeza rasilimali mbali mbali zitakazoiwezesha nchi kuanza mchakato wa ukarabati na ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi. Yote haya yanaweza kufanikiwa ikiwa kama wadau mbali mbali watajikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kudumisha amani ya kweli na inayodumu, ili kukoleza maboresho ya huduma za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Majadiliano ni njia pekee itakayoweza kunyamazisha mlio wa silaha za vita, tayari kuanza mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Bangui, ilitoa hamasa kubwa ya ushirikiano na umoja wa kitaifa sanjari na kudumisha majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali nchini humo. Amani ya kweli ni chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anakaza kusema, ili mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kuna haja ya kusitisha mapigano kati ya vikundi vinavyokinzana; kuwanyang’anya silaha wapiganaji na hivyo kuanzisha mchakato wa kuwaingiza katika mfumo rasmi wa kiraia na ujenzi wa jumuiya ya kidemokrasia. Haki inapaswa kutendeka kwa kuwafikisha wahusika wa mauaji ya kikatili kwenye mkondo wa sheria. Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuhakikishiwa usalama wao, ili waweze kurejea tena nchini mwao katika hali ya amani na utulivu. Katika mbinu mkakati huu, Kanisa linapenda pia kushiriki na kutoa mchango wake, kwa kuendeleza majadiliano ya kidini; ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa ili kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.