2017-09-21 15:13:00

Papa Francisko na mchakato wa mapambano dhidi ya vitendo vya Mafia


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 21 Septemba 2017 amekutana na kuzungumza na Tume ya Bunge la Italia dhidi ya Mafia, kwa kutoa heshima zake za dhati kwa Mahakimu waliojisadaka kusimamia ukweli na haki hawa ni pamoja na Mtumishi wa Mungu Rosario Livatino, aliyeuwawa kunako mwaka 1990, Giovanni Falcone na Paolo Borsellino waliouwawa miaka 25 iliyopita pamoja na baadhi ya watu waliokuwa kwenye msafara wao.

Baba Mtakatifu anasema, dhambi na ubaya vinapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, mahusiano na mambo ambayo anapenda kujishikanisha nayo! Mazingira yote haya yanamfanya mwanadamu kuwa ni kiumbe hatari sana hasa pale anapojifungia katika ubinafsi wake pamoja na kuelemewa na kishawishi cha kutumia kila fursa inayokuja mbele yake kwa ajili ya mafao binafsi na zaidi sana pale, mtu anapojiamini kupita kiasi. Yote haya yanatia ukungu katika dhamiri nyofu ya mtu, kiasi cha kugeuza dhambi kuwa ni jambo la mazoea; kwa kushindwa kuona ukweli pamoja na kutumia nafasi yake kama kiongozi wa umma kwa ajili ya kujinufaisha mwenyewe.

Baba Mtakatifu anasema, siasa, kimsingi ni huduma ya upendo, chemchemi ya matumaini na mchakato unaopania kulinda na kudumisha utu wa binadamu. Mapambano dhidi ya vitendo vinavyofanywa na kikundi cha kigaidi cha Mafia ni sehemu muhimu sana ya vipaumbele vya siasa nchini Italia ili kulinda mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Leo hii, rushwa ni tatizo kubwa la kijamii kwani inaunda mazingira yanayostawisha na kurutubisha vitendo vya kigaidi na matokeo yake ni utekaji nyara wa watu jambo ambalo baadaye linachukuliwa kuwa kana kwamba ni kitu cha kawaida.

Matokeo yake ni kuwakatisha watu tamaa ya kuwekeza nchini Italia. Kimsingi, vitendo vya mafia ni tabia inayofumbatwa katika uchu wa mali na fedha; kwa kugeuza utu na heshima ya binadamu kuwa kama bidhaa sokoni. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kupambana kufa na kupona na vitendo vya kigaidi vinavyosababishwa na kikundi cha Mafia. Baba Mtakatifu anasema, haitoshi kudhibiti vitendo hivi, bali kuhakikisha kwamba, mali inayotaifisha inawasaidia watu ndani ya jamii katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika utawala wa sheria. Shughuli za kisiasa hazina budi kuboresha zaidi haki jamii kwani mahali ambapo kunakosekana haki msingi katika masuala ya: kazi, nyumba, ujenzi na huduma za afya, hapo kikundi cha Mafia kinaweza kupenyeza mkondo wake.

Hatua ya pili anasema Baba Mtakatifu ni kuhakikisha kwamba, mchakato wa shughuli za kiuchumi unabomolea mbali miundo mbinu inayosababisha umaskini na ubaguzi; kwa kukataa kishawishi cha kutumia fedha katika masuala ya uchaguzi na ya kisiasa. Hii ni fedha inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia kwani inapatikana kutokana na biashara haramu ya binadamu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya silaha; uchakachuaji wa taka zenye sumu; takrima kwenye miradi mikubwa mikubwa ya kitaifa, michezo ya kamari na rushwa. Mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Mafia hayana budi kujikita katika dhamiri yenye ustaarabu; elimu makini na endelevu; kwa kutambua na kudhibiti fursa na mianya ya rushwa; kwa kujenga na kudumisha moyo wa uzalendo na utawala wa sheria; uwajibikaji kwa jirani na daima kusimamia mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu Francisko anaipongeza Serikali ya Italia kwa kuunganisha nguvu za kisheria na kiutawala zinazowaunganisha wananchi na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Mafia. Mali inayotaifishwa kutoka kwa Mafia, sasa inatumika kwa ajili ya ustawi wa wananchi wote, utu, heshima na huduma makini. Mapambano dhidi ya Mafia yanajikita pia katika ushuhuda unaolinda na kudumisha haki; kwa kukataa kukumbatia utamaduni wa kifo na ghasia kwa kuhakikisha kwamba, watoto wao wanaishi katika mazingira salama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.