2017-09-20 06:56:00

Vijana jitahidini kuwa waaminifu katika wito na maisha yenu!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika hija yake kitume, kama Mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan, Jumatatu, tarehe 18 Septemba 2017 amekutana na Majandokasisi kutoka Fukuoka na hatimaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Sehemu ya kwanza katika mkutano wake na Majandokasisi amekazia umuhimu wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu nchini Japan. Dhamana hii haina budi kwenda sanjari na utamadunisho unaofumbatwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali nchini Japan.

Wakristo wawe ni mashuhuda wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; chemchemi ya faraja, ukarimu na wema, kwani anataka watu wote waweze kuufahamu ukweli na hatimaye, waweze kuokoka! Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo kwa watu wote pasi na ubaguzi. Kanisa linapenda kuwahamasisha watu wote kumtafuta Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao, maadamu anapatikana. Kumbe, ni wajibu wa waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa upya wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Fernando Filoni anawataka majandokasisi kuondokana na utamaduni wa mambo mpito, kwa kujikita katika maamuzi magumu ya maisha, yanayowajibisha barabara. Katika ujana wao wakiamua kufunga ndoa, watambue kwamba, hii ndoa ambayo inadumu maisha yote kama ulivyo wito na maisha ya upadre na utawa. Wajitahidi kujisadaka kama vyombo na mashuhuda wa mchakato wa uinjilishaji wa familia ya Mungu ndani na nje ya Japan kama kielelezo kikuu cha upendo unaobubujika kutoka katika imani.

Vijana katika maisha yao, wajitahidi kutambua upendo wa kweli na wala si upendo ndoana, nipe nikupe! Vijana wanapaswa kuwa waaminifu katika maisha yao, kwa kuzingatia na kuambata mambo msingi katika maisha ya mwanadamu. Wawe ni mashuhuda na vyombo makini vya upendo wa dhati kati ya watu wa Mataifa. Wasikubali kupigishwa magoti na vitendo vya rushwa na ufisadi, bali wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Katika maisha yao, wawe ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ndani na nje ya Japan kama walivyofanya wamisionari, wafiadini na waungama imani kutoka Japan.

Wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, Kardinali Fernando Filoni kwenye mahubiri yake, amekazia umuhimu wa sala katika maisha ya waamini. Changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, ikipewa kipaumbele cha kwanza, kama Yesu alivyomponya yule mtumwa wa Akida. Viongozi katika medani mbali mbali za maisha waoneshe na kushuhudia fadhila ya unyenyekevu; kwa kuwajali na kuwasikiliza maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao na kwamba, Habari Njema ya Wokovu ni zawadi inayotolewa kwa binadamu wote pasi na ubaguzi. Wokovu wa Mungu kwa binadamu ni kazi iliyotekelezwa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Kardinali Filoni ametumia fursa hii kuwasilisha pia salam, baraka na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Seminari ya Fukuoka, nchini Japan.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.