2017-09-20 16:00:00

Padre Gregory Mashtaki aguswa sana na katekesi ya Papa Francisko!


Padre Gregory Mashtaki kutoka Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania, ni kati ya waamini waliohudhuria katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Septemba, 2017 hapa mjini Vatican. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, anamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aliyemwezesha kupata nafasi ya kutembelea mjini Vatican na kupata nafasi ya kumwona na kumsikiliza Baba Mtakatifu Francisko mbashara! Matendo makuu ya Mungu! Sasa anaweza kumruhusu mtumishi wake aende zake kwa amani!

Padre Mashtaki ambaye amekwisha kula chumvi nyingi katika maisha na utume wa Kipadre anasema, ameguswa sana na katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye anawataka waamini kusimama imara katika tumaini lao kwa Mwenyezi Mungu na kamwe wasikate tamaa kwani atayafanya yote kuwa mapya. Waamini wawe wadumifu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao; kwa kudumisha mwanga wa imani, matumaini na mapendo ndani mwao, ili kwa njia yao nuru ya mwanga wa Injili iweze kuwafikia wote na hatimaye, watu wote wapate kuokoka!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kukuza na kudumisha: uhuru, haki, amani duniani. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake na hasa katika ulimwengu huu ambao unaelemewa sana na ubinafsi, dhambi na maovu mbali mbali, ili kuwasaidia watu waweze kuishi kwa matumaini zaidi. Baba Mtakatifu anawataka waamini kusimama na kutoka kifua mbele ili kuwaangazia wote waliokata tamaa matumaini ya Kikristo; kwa kuishi vyema, kuwapenda na kuwathamini binadamu wote, kwani hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, wazidi kudumu katika imani na matumaini kwani kwa njia ya neema ya Mungu, iko siku watafanikiwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.