2017-09-20 15:04:00

Familia ya Mungu nchini Japan inahamasishwa kuwa ni shuhuda wa Kristo


Familia ya Mungu nchini Japanwanatakiwa kuwa ni shuhuda wa Kristo Yesu anayepaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa na ari na mwamko mpya katika mchakato wa uinjilishaji mpya kati ya watu wa Mataifa. Vijana wanakumbushwa kwamba, wito ni safari ya maisha inayomtaka mwamini kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa kutumainia ulinzi na tunza yake ya kibaba! Waamini waoneshe huruma na mapendo kwa jirani zao, wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha!

Kwa muhtasari haya ndiyo mawazo makuu yaliyotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika ziara yake ya kikazi nchini Japan, Jumanne, tarehe 19 Septemba, 2017. Akiwa mjini Nagasaki, Kardinali Filoni amekutana na kuzungumza na Wakleri, Majandokasisi na hatimaye, akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Nagasaki, Japan.  Katika hija hii, Kardinali Filoni anafuatana na Askofu mkuu Joseph Mitsuaki Takami wa Jimbo kuu la Nagasaki pamoja na Askofu mkuu Joseph Chennoth, Balozi wa Vatican nchini Japan.

Sakramenti ya Ubatizo inawajalia waamini kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu na hivyo kupatiwa utambulisho wao kama Wakristo, yaani wafuasi wa Kristo! Kwa Ubatizo wanauvua utu wao wa zamani na kujivika utu mpya, unaowawezesha kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka anayewawezesha wote kujisikia kuwa ni watoto wa Baba mmoja. Utambulisho huu mpya ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga ili kuambatana na kushikamana na Kristo Yesu kama alivyofanya Mwenyeheri Justus Takayama Ukon kiasi hata cha kuachilia yote ili kumwambata Kristo Yesu katika maisha yake. Hii ni changamoto inayohitaji kumwilishwa katika mchakato wa utamadunisho ili kukabiliana na changamoto mamboleo.

Wakristo nchini Japana wanapaswa kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; kwa njia ya huduma ya upendo na mshikamano; kwa kusimamia haki msingi, utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hakuna umaskini mkubwa katika maisha ya watu, kama kutomfahamu na kumpenda Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Huu ni mwaliko kwa waamini nchini Japan kuwa na ari na mwamko mkubwa wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa maisha yao. Wasimame kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na kuhakikisha kwamba maisha yao yanaongozwa na kanuni maadili na utu wema. Katika utekelezaji wa dhamana na utume wa kimisionari, watambue kwamba, wanaweza kukumbana na madhulumu kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu na hata wakati huu sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Fernando Filoni anapenda kuwatia shime kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika maisha yao, licha ya shida, magumu ya maisha na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo kila siku! Kazi kubwa imekwisha kutekelezwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya neema na baraka zake. Haya ndiyo matumaini ya Kanisa ambayo hakuna mtu awaye yote anaweza kuwapokonya katika katika maisha yao

Akizungumza na Majandokasisi, Kardinali Filoni amewakumbusha kwamba, wito ni hija ya maisha inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama alivyofanya kwa Abrahamu, Baba wa imani; Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, Mtakatifu Francisko Xsaveri, Paulo Miki na wenzake, Mama Theresa wa Calcutta na watakatifu wengineo ndani ya Kanisa. Wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni safari ya imani kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Dhamana hii inawataka waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.

Ni safari inayojikita katika toba na wongofu wa ndani kama iliyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Mwenyezi Mungu anatambua udhaifu na karama zao zinazoweza kutumika kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Waamini wakumbuke kwamba, watakatifu ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu katika hija ya maisha yao, hali inayodai ujasri na unyenyekevu kama ilivyokuwa kwa Watakatifu Petro na Paulo.

Kardinali Filoni katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa waamini kuwa ni mashuhuda wa upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini waone, waguswe na kuwajibika kama vyombo na mashuhuda wa wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mtakatifu Francisko Xsaveri awe ni mfano bora wa kuigwa kwa kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa. Waamini washuhudie kanuni maadili na utu wema; wawe ni vyombo vya huduma makini kwa watu wanaoteseka: kiroho na kimwili.

Kimsingi, Kanisa linawataka Wakristo nchini Japan kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kiini cha imani na matumaini ya Kanisa. Kristo Yesu, ni ufuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu! Kumbe, huu ni wajibu wa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebwe kupambana na umaskini wa hali na kipato; kukataa kishawishi cha uchu wa fedha, mali na madaraka; kwa kupinga utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Wakristo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na mapendo; haki na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.