2017-09-20 14:19:00

Dalai Lama:Anayeua ni gaidi siyo dini na kuishi kwa amani inawezakana


Kiongozi mkuu wa dhehebu la wabudha Tenzin Gyatso ajulikanaye Dalai Lama ni mgeni wa Jukwaa la Nelson Mandela huko Firenze, mji maarufu sana wa kisanaa wa  Mkoa  wa Toscana nchini Italia ili kufungua toleo la tatu la Tamasha ya kidini kuanzia tarehe 19 hadi 23 Septemba 2017. Katika tukio hilo, Meya wa mji wa Firenze Dario Nardella amemtunuku muhuri wa amani wa kizamani. Wakati wa kumtunuku zawadi hiyo Meya wa mji amesema, furaha yake ya kumtunuku zawadi ya kihistoria iliyotengenzwa karne ya XV kwa niaba ya jumuiya ya wazalendo wa mkoa wa Toscana Italia, kama ishara ya amani na uhuru kwasababu hakuna uhuru bila kuwa na amani.

Naye Dalai Lama wakati wa kutoa hotuba yake ikiwa ni baada ya miaka 20 tangu akanyage mguu katika mji wa Firenze anasema, kuna dini nyingi duniani ambazo hubeba falsafa tofauti, lakini tofauti hizi ni msingi na siyo tatizo. Je, kunaa uwezekano wa kuishi kwa utulivu na amani duniani?. Anathibitisha kuwa, inawezakana. Kwa kuendelea ametoa mfano wa bara lake kwamba: Kwa mfano, nchini India  ni zaidi ya miaka elfu sasa , dini zote na tamaduni huishi pamoja kwa amani. Sisi ni jamii moja ya bilioni 7 za wanadamu; ni lazima tuwe pamoja ili kukuza upendo wa ulimwengu wote; amani ya ulimwengu wote na msamaha wa ulimwengu. Aidha anaongeza: ni jambo lisiloelezeka  kusikia kwamba dini ni chanzo cha migogoro, na kwa njia hiyo ugaidi siyo dini. Dini na ugaidi havipaswi kulinganishwa pamoja, ni vitu viwili tofauti japokuwa mara nyingi inajitokeza kukuambatanisha migogoro ya magaidi na  dini.

Halikadhali anaongeza mfano mwingine kuwa, watu wengine wanaongea kwa mfano ugaidi wa kiislam , au ugaidi wa Wabudha. Kwa upande huo Dalai Lama anasema yeye anapinga neno hilo ,kwa sababu ikisha julikana jina la ugaidi siyo tena dini kwasababu unapofanya tendo la kuua, wewe siyo mtu wa  dini bali wewe ni gaidi tu, amethibitisha kiongozi wa Kiroho na siasa kutoka Tibet.

Katika mkutano huo wameudhuria hata Padre Enzo Binanchi Mwanzilishi wa Jumuiya ya Kiekumeni ya Bose kwa  watawa  wa  kike na kiume  kutoka katika Makanisa mbalimbali ya kikristo wakiishi kwa pamoja. Aidha Imamu wa Kiislam Izzedin Elzir huko Firenze na ni Mwenyekiti wa Umoja wa Jumuiya ya Kiislam nchini Italia.Kiongozi huyo akitoa neno juu ya dini na ugaidi amesema,  ugaidi kwa kutumia jina la Mungu ni kukufuru dini na imani ya kidini, kwa njia hiyo Imam Elzir anawaalika wote kwa namna ya pekee hata waandishi wa habari wasihusishe ugaidi na dini yoyote, badala yake, lazima kufanya kazi kubwa  wote ili kujaribu kuwa macho wakati wote kwasababu ugaidi kwa bahati mbaya leo hii unashangaza kila mahali, hivyo ni  kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kwenda zaidi ya kushinda hofu.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.