2017-09-19 16:54:00

Waamini onesheni huruma kwa kuguswa na mahangaiko ya jirani zenu!


Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alionesha huruma, akawakaribia watu katika shida na mahangaiko yao, akawarejeshea tena maisha, utu na heshima yao. Hii ndiyo changamoto ambayo bado inawakabili Wakristo wanaopaswa kumwomba Mwenyezi Mungu ili awajalie neema na baraka kuwakaribia wale wote wanaoteseka, ili kuwagusa kwa mikono yao, tayari kuwarejeshea tena ule utu na heshima ambayo Mwenyezi Mungu anataka kuwakirimia tena katika maisha. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 19 Septemba 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Mwinjili Luka anasimulia kisa cha Kristo Yesu, kumfufua kijana wa Naini, baada ya kumwonea huruma yule mwanamke mjane aliyefiwa na mtoto wake wa pekee. Ikumbukwe kwamba, wajane na watoto yatima na wageni katika Agano la Kale walihesabika kuwa ni kati ya maskini sana ambao, familia ya Mungu ilipewa jukumu la kuhakikisha kwamba, inatoa huduma makini kwa watu hawa kama kielelezo cha ukarimu unaobubujika kutoka katika imani yao kwa Mwenyezi Mungu. Yesu, aliyekuwa na uwezo wa kuangalia undani wa mtu, akamwonea mwanamke yule mjane huruma, akagusa maiti ya mtoto wake, akamponya na kumrudishia tena mama yake.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na jicho la huruma wanapoangalia matukio mbali mbali katika maisha ya watu, tayari kushiriki na kugusa ukweli wa mambo badala ya kuwa kama watazamaji wasioguswa na mahangaiko ya watu! Yesu alimwonea huruma; akamkaribia, akaligusa jeneza na kutenda muujiza wa kumfufua yule kijana na hatimaye, akamrudishia tena yule mwanamke akiwa hai. Hivi ndivyo Kristo Yesu alivyofanya kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti; akawarejeshea tena ile heshima na utu wa wana wateule wa Mungu. Hii ndiyo changamoto ya kuwaendelea na kuwagusa watu na hatimaye, kuwasaidia katika shida na mahangaiko yao.

Waamini wasiwe watazamaji, wanaosikitishwa na matukio mbali mbali yanayotendeka sehemu mbali mbali za dunia, bila kujishughulisha hata kidogo. Ni vyema, ikiwa kama waamini watajiuliza swali la msingi, ikiwa kama kweli wana huruma, wanaweza kusali na kujishughulisha kadiri ya nafasi na uwezo wao yale wanayoyaona yakitangazwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Haitoshi kuwaonea watu huruma, bali kuchukua hatua madhubuti ili kuwasaidia. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kuwa na huruma ya kuwasaidia wale wanaoteseka: kiroho na kimwili. Wakristo kwa njia ya maisha na utume wao, wawe na ujasiri wa kuwasaidia watu wanaoteseka, ili kuwarejeshea tena utu, heshima na dhamana katika maisha yao ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.