2017-09-18 08:48:00

Kanisa nchini Japan limesimikwa katika msingi wa damu ya mashuhuda!


Umuhimu wa ushuhuda wa imani uliotolewa na wafiadini wa Kanisa nchini Japan, akina Paulo Miki na wenzake; mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini, umuhimu wa ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uaminifu kwa Injili ya Kristo na Kanisa lake, malezi na majiundo makini kwa wakleri na watawa ndani ya Kanisa; haya ni mambo mazito ambayo Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Maaskofu Katoliki nchini Japan, wakati huu, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anapofanya safari ya kitume nchini Japan, kuanzia tarehe 17 hadi 26 Septemba 2017.

Baba Mtakatifu anaikumbuka hija ya kitume iliyofanywa na Maaskofu Katoliki Japan kunako mwaka 2015, daima akilini mwake kumebakia ile picha ya mashuhuda wa imani walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hawa si wengine ni wafiadini Paulo Miki na wenzake waliouwawa kikatili kunako mwaka 1517. Anawakumbuka waungama imani kama Mwenyeheri Justus Takayama Ukon aliyekubali kukumbatia ufukara kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kuliko kumwasi Mungu.

Bado kuna umati mkubwa sana wa waamini walioungama imani yao kwa kificho kati ya mwaka 1600 hadi mwaka 1800, hao ndio ambao Kanisa limeadhimisha kumbu kumbu yao ya miaka 150. Umati mkubwa wa watakatifu, wafiadini na waungama imani kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni mashuhuda wa imani na upendo kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuacha yote ili kumwambata Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai!

Familia ya Mungu nchini Japan imebahatika kuwa na amana na urithi mkubwa wa maisha ya kiroho, unaoweza kuwasaidia kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Maaskofu Katoliki Japan kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kitamaduni, kidini sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Familia ya Mungu nchini Japana inapaswa kutambua kwamba, Kanisa Katoliki lina dhamana na wajibu wa kimisionari unaofumbatwa katika upendo wa Kristo unaowawajibisha kutangaza na kushuhudia Injili, kiasi hata cha kujisadaka bila ya kujibakiza.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki nchini Japan kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa ili kukoleza mchakato wa huduma makini kwa watu wa Mungu nchini Japan. Kanisa lazima liwe mbali sana na rushwa pamoja na ufisadi, kwa kuonesha dira na mwanga wa maisha! Kanisa halina budi kua aminifu kwa tunu msingi za Kiinjili ili kushinda giza la dhambi. Kanisa katika maisha na utume wake, liwe ni shuhuda wa ufukara, makini katika utekelezaji wa utume wake: kiroho na kimaadili. Baba Mtakatifu anatambua vyema, ukame wa wakleri na watawa pamoja na ushiriki mdogo wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanajitaabisha kutafuta watenda kazi katika shamba ya Bwana, bila kukata wala kukatishwa tamaa na hali halisi ya maisha ya ndoa na familia kutokana na kiwango kikubwa cha wanandoa wanaotalikiana kila kukicha kiasi cha kudhohofisha Injili ya familia. Nchini Japan, anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna kiwango kikubwa cha vijana wanaotema zawadi ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo! Kuna baadhi ya waamini ambao hawaoni tena umuhimu wa kujihusisha na maisha ya kijamii; kuna watu ambao wamekengeuka na kugubikwa na ubaridi wa maisha ya kiroho kwa kumezwa mno na mahangaiko ya kutafuta fedha, mali na kazi.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, pamoja na maendeleo makubwa ya uchumi, bado kuna maskini wa hali na kipato; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto kwa Kanisa nchini Japan ni kujipyaisha, ili liweze kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa! Hili ni Kanisa ambalo limesimikwa katika msingi wa mashuhuda wa imani na wafiadini, nguzo imara katika ujenzi, utunzaji na maendeleo ya Kanisa la Kristo! Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja ya kuwa na majiundo makini ya awali na endelevu kwa wakleri na watawa nchini Japan, ili kuondokana na utamaduni wa mambo mpito usiokuwa na tija wala mashiko kwa maisha na utume wa Kanisa.

Vijana wafundwe na kuaminishwa kwamba, inawezekana kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa kupenda kwa dhati na kudumu katika Injili ya familia, hadi pale kifo kinapowatengenanisha. Wakleri na watawa wawasaidie vijana katika hija ya maisha yao, lakini changamoto hii wanaweza kuivalia njuga, ikiwa kama hata wao wenyewe wamefundwa imara, kukumbatia upendo wa Kristo unaosimikwa katika undani wa maisha yao, kiasi hata cha kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Familia ya Mungu nchini Japana ina kiu ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuvitia shime vyama vya kitume ambavyo vimeidhinishwa na Vatican, ili viendelee kutekekeza dhamana na wajibu wake katika mchakato wa uinjilishaji na ushuhuda amini kwa Kristo na Kanisa lake. Vyama hivi viwe ni msaada mkubwa katika huduma makini na uinjilishaji wa watu na kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na mwamko mkubwa wa waamini wanaotaka kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, mwaliko ni kwa waamini hawa kuhakikisha kwamba, wanaishi kikamilifu umisionari wao ndani ya Kanisa, tayari kushikamana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda makini wa imani tendaji.

Kama Maaskofu na viongozi wa Kanisa wanapaswa kutambua, kung’amua na kusaidia kuendeleza karama hizi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa kama sehemu ya mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka Maaskofu wote wa Japan chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na kwamba, anawahakikishia uwepo wake wa daima kwa njia ya sala, ili kweli Bwana wa mavuno aweze kupeleka watenda kazi katika shamba lake nchini Japan. Anawashukuru kwa huduma yao makini kwa familia ya Mungu nchini Japana na mwishowe, anawapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.