2017-09-18 09:21:00

Askofu mkuu Gallagher: Changamoto za Jumuiya ya Kimataifa: Usalama!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Myanmar na Bangaladesh, mwishoni mwa Mwezi Novemba 2017 kama kielelezo cha mshikamano wake na watu wa familia ya Mungu wanaoteseka katika maeneo haya, ili kuwashirikisha upendo na faraja, inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hatima ya wakristo huko Mashariki ya kati, changamoto ya amani na usalama katika Jumuiya ya Kimataifa, baada mashindano ya majaribio ya kurusha makombora ya masafa marefu kutoka Korea ya Kaskazini pamoja na mchango wa Iran katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa kivita huko nchini Syria na Iraq ni kati ya mambo ambayo yamefanyiwa kazi na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican katika safari yake ya kikazi aliyoihitimisha hivi karibuni huko Iran, na kubahatika kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Iran.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakiri kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Aung San Suu Kyi, Kiongozi kutoka Myanmar, mwezi Mei, 2017 aligusia kuhusu mateso na mahangaiko ya watu wa Rohingiya. Baraza la Maaskofu Katoliki Myanmar linasema, litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za jamii ya watu wa Rohingiya ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha, baada ya vikosi vya ulinzi na usalama kuchoma vijiji kadhaa na kuwashambulia watu, kiasi cha kulazimika kuyakimbia makazi yao ili kutafuta: hifadhi na usalama. Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Myanmar inapaswa kuvaliwa njuga na wadau wote kwa kuonesha ujasiri. Baba Mtakatifu Francisko anaguswa sana na mateso, mahangaiko pamoja na hatima ya wakimbizi sehemu mbali mbali za dunia!

Amezungumzia pia hatima ya maisha ya Wakristo huko Mashariki ya Kati na kwamba, kuna haja ya kusimamia haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu kama chachu ya ujenzi wa amani na usalama huko Mashariki ya Kati. Wakimbizi kutoka Syria wanaohifadhiwa nchini Lebanon na Yordan, wataweza kurejea tena nchini mwao, ikiwa kama amani na utulivu vitarejeshwa tena huko Siria na vijiji vyao kuanza kufanyiwa ukarabati mkubwa, kwa ajili ya maisha ya watu, lakini hali kama ilivyo kwa sasa ni vigumu sana. Ikumbukwe kwamba, Wakristo wanao mchango mkubwa sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi huko Mashariki ya Kati, kumbe, si Jumuiya inayopaswa kubezwa wala kudhalilishwa. Ni sementi inayounganisha jamii na kwamba, wanapaswa kuwa sehemu ya maisha ya watu wa Mashariki ya Kati na kamwe wasionekane kama ni “watu wa kuja”.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher amezungumzia kuhusu hali ya maisha na utume wa Wakristo nchini Iran, kwa kukazia uhuru wa kuabudu, ushuhuda wa Wakristo katika ujenzi na ustawi wa nchi yao na kwamba, Serikali ya Iran inashukuru sana mchango unaotolewa na Wakristo nchini humo, licha ya kwamba, dini ya Kiislam ndiyo dini rasmi ya Serikali ya Iran. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Serikali ya Iran itaongoza juhudi za ushirikiano na Kanisa kwa ajili ya maendeleo ya wengi, ikiwa ni pamoja na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu, matatizo na changamoto zinazowakabili Wakristo huko nchini Iran. Wazo la Papa kutembela nchini Iran bado ni ndoto ya kufikirika sana, kwani jambo la msingi kwa wakati huu, ni ule uhusiano mzuri ulipo kati ya Serikali ya Iran na Vatican ushuhudiwe pia kwa Kanisa mahalia.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anasikitika kusema kwamba, amani, usalama na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa viko mashakani kuliko hata ilivyokuwa pengine kabla ya Vita kuu ya Pili ya Dunia. Korea ya Kaskazini na uwezo wake wa kijeshi unatishia usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Vatican inaendeleza msimamo wake wa kutaka kuona dunia inaondokana na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia ambayo ni hatari sana kwa wakati huu. Ili kuweza kufikia lengo hili, Askofu mkuu Gallagher anasema, kuna haja ya kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kanuni maadili yanayosimikwa katika haki, amani na udugu badala sera na mbinu mkakati wa vitisho vinavyoamsha hasira na ghadhabu za watu, hali inayoweza kuchafua hali ya usalama na amani duniani kwani vita haina macho wala pazia!

Ni matumaini ya Vatican kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupata suluhu ya mpasuko wa kisiasa huko Korea ya Kaskazini kwa njia ya majadiliano. Kwa muda wa miaka 20 sasa, mawasiliano ya kidiplomasia kati ya Korea ya Kaskazini na Vatican yanasuasua sana. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuangalia machafuko haya kwa mapana zaidi kwani yanatishia amani, usalama na ustawi wa Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.