2017-09-18 16:19:00

Askofu Kilain:Kijana aliyepokea kipaimara ni askari wa Kristo


Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba nchini Tanzania  amesema, wazazi na wasimamizi wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuwaelekeza watoto wao ili waendelee kuyashika waliyofundishwa. Amesema hayo wakati wa mahubiri yake kwenye  Misa Takatifu katika Parokia ya Watakatifu wote Kiluvya Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Tanzania mapema wiki iliyopita ambapo vijana 115 wamepokea Sakramenti ya Kipaimara.

Katika mahaubiri anasema,Kipaimara ni Sakramenti ya ishara ya ukomavu wa kikristo na mafuta ya Krisma inaacha alama isiyofutika na kupokea Roho Mtakatifu mioyoni mwao. Kijana anayepata kipaimara tayari ni askari wa Kristo kwa sababu anayo mawazo mazuri, matendo mazuri, fikra nzuri katika kujituma kutekeleza tendo lolote linalotendeka kadili ya miongozo ya Kanisa. Askofu anasisitiza kuwa, mwanakipaimara kamwe hasione haibu kutaja maneno ya Mtume Paulo yasemayo, kuishi kwangu ni Kristo.Pamoja na hayo amewataka wazazi na walezi au wasimamizi wa vijana ambao wamepewa Kipaimara wanatakiwa kuendelea kuwalea vijana hao kwa maana ya mafundisho waliyoyapata hayatoshelezi hali halisi ya imani yao bali kuendelea kuwaelekeza katika kumshuhudia Kristo.

Na hiyo ni kwasababu, ili kutengeneza jeshi la Kristo lazima malezi bora yaanzie ngazi ya familia ambayo ndiyo msingi wa maisha ya kizazi endelevu. Mazingira ya nyumbani yakiandaliwa vizuri hasa wazazi kwa kusali pamoja, kufanya maamuzi ya busara kwa pamoja hata na watoto watakuwa na hekima katika kuishi maadili yao. Pia wazazi wametakiwa kutofumbia macho mambo maovu ambayo yanaweza kuchangia upotovu wa watoto wao kuzama katika ulimwengu wa maovu na badala yake kuwafundisha vijana wao misingi ya Kanisa Katoliki na kuishikilia vema katika maisha yao.

Sr Angela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya  Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.