2017-09-16 14:16:00

Kuna watu milioni 815 wanateseka kwa baa la njaa na utapiamlo mkali


Takwimu za hali ya usalama wa chakula na lishe duniani kwa Mwaka 2017 zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna watu milioni 815 wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani kwa takribani kipindi cha miaka kumi iliyopita. Idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana na njaa na lishe duni kwa mwaka 2016 imeongezeka maradufu, sawa na asilimia 11% ya idadi ya watu duniani wanakabiliwa na baa la njaa. Kuna ongezeko la watu milioni 38 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2016. Haya ni matokeo ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto milioni 155 wenye umri chini ya miaka 5 wanaokabiliwa na tatizo la kudumaa; wengine milioni 52 wanateseka kutokana na athari za utapiamlo wa kutisha waliokumbana nao katika maisha. Lakini kuna watoto 41 ambao wana uzito wa kupindukia. Zote hizi ni athari pia zinazosababishwa na mabadiliko makubwa ya mfumo wa chakula na lishe duniani pamoja na kusuasua mwenendo wa ukuaji wa uchumi duniani. Umoja wa Mataifa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ifikapo mwaka 2030 unapania kumaliza baa la njaa duniani! Lakini kwa takwimu za hivi karibuni, ni mapema mno kuweza kusema ikiwa kama lengo hili litaweza kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa kutokana na sababu mbali mbali.  Bara la Afrika lina watu milioni 243 wanaoteseka kwa baa la njaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.