2017-09-16 13:26:00

Caritas Africa: Huduma ya upendo Barani Afrika


Kanisa katika ulimwengu mamboleo linapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; matendo ya huruma kiroho na kimwili ni mambo msingi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji. Upendo wa Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kuwa upendo wa kibinadamu unapata utimilifu wake katika upendo wa kimungu. Upendo huu unatafsiriwa kwa lugha ya Kigiriki kuwa ni Agape, kwa Kilatini, Caritas. Kanisa linapenda kukazia huduma ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wake na kwamba, upendo wa Kimungu unalikamilisha na kuliwezesha Kanisa kusimama kwa miguu yake.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako tarehe 11 Novemba 2012 katika Barua yake binafsi “Intima Ecclesiae Natura” yaani “Huduma ya upendo ni asili ya Kanisa” alikazia mambo makuu matatu: Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu “Kerygma-martyria; maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa “Leiturgia” na huduma ya upendo “Diakonia”. Haya ni mambo makuu matatu yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa.

Waamini wote wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanayamwilisha yote haya katika maisha yao kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa Amri ya upendo kwa Mungu na jirani. Huduma ya upendo haina budi kugusa maeneo yote ya maisha ya waamini kuanzia katika ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi katika ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Kutokana na changamoto hii, kuna haja ya kuwa na miundo mbinu itakayosaidia utekelezaji wa Amri ya upendo kati ya watu!

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anaendelea kufafanua kwamba, huduma ya upendo inatekelezwa kwa namna ya pekee kabisa na Mama Kanisa kwa njia ya Maaskofu mahalia ambao ni waandamizi wa Mitume wa Yesu na kwamba, huu ni utume maalum kwa Maaskofu mintarafu Sheria za Kanisa. Kumbe, Barua binafsi ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI “Intima Ecclesiae Natura” yaani “Huduma ya upendo ni asili ya Kanisa” anafafanua jinsi ya utekelezaji wa huduma hii katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi; upendo na mshikamano mintarafu tunu msingi za Kiinjili pamoja na ushirikishwaji wa waamini wote kila mtu kadiri ya uwezo na nafasi yake.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 17 Agosti 2016 kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa katika Sekretarieti ya Vatican, alichapisha Barua binafsi inayojulikana kama “Humanam Progressionem” yaani “Maendeleo endelevu ya binadamu”, iliyoanzisha Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu mintarafu mwanga wa Injili. Haya ni maendeleo yanayofumbatwa katika haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kusikiliza na kujibu kwa ufasaha kilio cha mahitaji msingi ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Ni Baraza linalojikita katika huduma ya afya ya binadamu pamoja na kuratibu Mashirika yote ya Misaada ya Kanisa Katoliki. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linawasaidia na kuwahudumia wakimbizi, maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha.

Nyaraka hizi mbili yaani: “Intima Ecclesiae Natura” yaani “Huduma ya upendo ni asili ya Kanisa” pamoja na “Humanam Progressionem” yaani “Maendeleo endelevu ya binadamu” ndizo zinazofanyiwa kazi na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika, Caritas Afrika katika mkutano wake unaoanza tarehe 17-21 Septemba 2017 huko Dakar, Senegal kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kuratibu Huduma ya Upendo Barani Afrika: Wajibu wa Maaskofu” mintarafu nyaraka hizi mbili zilizotolewa hivi karibuni! Kardinali Peter Turkson na Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa ni kati ya “vigogo” kutoka Vatican wanaoshiriki katika mkutano wa Caritas Afrika.

Mada nyingine zinazo chambuliwa katika mkutano huu ni pamoja na “Mwelekeo wa kijamii katika mchakato wa uinjilishaji; umuhimu wa Waraka wa Kichungaji wa Papa mstaafu Benedikto XVI, ”Deus Caritas Est” yaani  “Mungu ni upendo”; Uratibishaji wa huduma ya upendo inayotolewa na Kanisa ndani ya Kanisa sanjari na uwepo wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu na dhamana yake katika Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa. Kutakuwepo na taarifa kutoka katika Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kutoka katika baadhi ya Nchi za Kiafrika.

Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika yatashirikisha mchango wake katika huduma ya upendo kwa watu wa Mungu Barani Afrika, bila kuwasahau wadau wa maendeleo endelevu Barani Afrika. Umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na mchakato wa kujenga na kudumisha amani Barani Afrika. Itakuwa ni nafasi ya kujadiliana pia na Mashirika ya Misaada ya Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na mashirika ya kimataifa. Kuangalia uwezo, mafanikio, udhaifu na mapungufu ya Mashirika ya Caritas Barani Afrika. Caritas Afrika, mwishoni itatoa tamko lake mintarafu mkutano huu ambao utafungwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.