2017-09-15 12:39:00

Ni wanawake peke yao wenye ujasiri wa kusimama chini ya Msalaba


Mama Kanisa baada ya kuadhimisha Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba, hapo tarehe 14 Septemba, siku inayofuatia, yaani tarehe 15 Septemba anafanya pia kumbu kumbu ya Bikira Maria, Mama wa wa mateso aliyethubutu kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, akiinamisha kichwa na kukata roho! Katika mazingira ya mateso na majonzi makuu, wanawake pekee,  ndio waliothubutu kubaki chini ya Msalaba kushuhudia tukio la ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Hata leo hii, wanawake wanao ujasiri mkubwa wa kuweza kuandamana na watoto wao katika mateso na mahangaiko yao, daima wakiwaenzi kwa fadhila ya matumaini.

Hii ni sehemu ya mahubiri iliyotolewa na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa mateso kwenye Madhabahu ya Siracusa. Bikira Maria alithubutu kumfuasa Mwanaye mpendwa katika Njia ya Msalaba na hatimaye, akasimama chini ya Msalaba, akiwa anatiwa shime na wanawake wenzake: akakesha, akasali na kumwombolezea Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Akaonja mateso na mahangaiko ya Mwana wa Mungu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Bikira Maria akatokwa na machozi kwa ajili ya mateso na Mwanaye, lakini zaidi kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Kutokana na ujasiri huu, Bikira Maria anakuwa kweli ni mwombezi wa wale wote wanaoteseka na kuomboleza kutokana na Misalaba mbali mbali wanayoibeba katika safari ya maisha yao hapa duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika fumbo la mateso na mahangaiko ya binadamu, daima anamwomba Mwenyezi Mungu kumkirimia neema na baraka ya kuweza kulia pamoja na wale wanaoteseka, hii ndiyo miwani sahihi inayomwezesha mwamini kumwona Kristo Yesu katika mateso na mahangaiko ya jirani zake. Yesu katika mateso na mahangaiko ya watu alithubutu kuangua kilio!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kili ona machozi ya viongozi wa Kanisa ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, pasi na kutumbukia katika kishawishi cha unafiki. Katika shida, magumu na mahangaiko mbali mbali ya maisha, waamini hawana budi kutambua kwamba, safari ya maisha yao, daima itafumbatwa katika mateso na mahangaiko, lakini imani na matumaini ya Kikristo yanawaalika waamini kuinua macho ya imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, anayewasubiri ili kuwapangusa machozi yao na kuyafanya mambo yote kuwa mapya anasema Kardinali Beniamino Stella.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.