2017-09-15 13:01:00

Mkutano wa vijana kimataifa: Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu 2018


Dhamana na wajibu wa vijana katika masuala ya kisiasa; utambulisho wa vijana wa kizazi kipya katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia; wakimbizi na wahamiaji; mahali pa majiundo awali na endelevu katika maisha na utume wa vijana ndani ya Kanisa ni kati ya tema zilizopembuliwa kwa kina na mapana na washiriki wa mkutano wa vijana kimataifa uliofanyika kuanzia tarehe 11- 15 Septemba 2017 hapa mjini Vatican.

Itakumbukwa kwamba, mkutano huu wa kimataifa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mwezi Oktoba 2018 mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii ni nafasi ya pekee kwa Maaskofu kuwasikiliza vijana kwa makini ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa utume kwa vijana wa kizazi kipya kwa kutambua karama na utajiri wao; matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika hija ya maisha yao ya ujana, kwani ujana ni mali, eti fainali uzeeni!

Kilio cha vijana wa kizazi kipya linapaswa kusikilizwa na kupewa majibu muafaka na Kanisa, kwa kuwapatia vijana utambulisho wao makini katika maisha na utume wa Kanisa; wawe ni sehemu muhimu sana ya majadiliano katika jamii, ili kuwajengea uwezo katika kuamua na kupambana na changamoto za maisha. Miundo mbinu ya mawasiliano, mahusiano na mafungamano ya kijamii si rafiki sana kwa maisha na utume wa vijana! Ulimwengu wa utandawazi una mafao yake makubwa, lakini pia unaleta changamoto nyingi kwa vijana wa kizazi kipya, kiasi cha kuwafanya kukosa: dira, utambulisho na mwelekeo sahihi katika maisha.

Vijana katika ulimwengu wa siasa wanao mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hawa ni sehemu muhimu sana inayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu unaoweza kuisaidia katika mchakato wa kupyaisha jamii; kwa kushirikishwa zaidi, katika mfumo unaozingatia: ukweli, uwazi pamoja na uwezo wa kufanya maamuzi mazito katika maisha. Lakini, kwa bahati mbaya, vijana wamekuwa pia wakitumiwa na wajanja wachache katika siasa kwa ajili ya mafao yao binafsi kiasi hata cha kusababisha cheche za mipasuko ya kinzani za kijamii. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutambua kwamba, vijana ni rasilimali katika mchakato wa uzalishaji na huduma katika dunia, kumbe wanapaswa kufundwa barabara katika ukweli na uwazi, uzalendo, kanuni maadili na utu wema. Vijana wa kizazi kipya, wanawahimiza “vijana wa zamani” kuwa na imani nao, kwani wana nguvu na utashi wa kuweza kushinda ubaya na dhambi, ingawa mara nyingi wao ndio waathirika wa kwanza. Vijana wajitahidi kuisikiliza sauti ya Kanisa ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.