2017-09-14 07:00:00

Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba wa Yesu: Utakatifu, huruma na upendo


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba, anaadhimisha Siku kuu ya Kutuka kwa Msalaba ambayo inapata chimbuko lake kunako mwaka 335 Mfalme Costantino alipojenga Makanisa makuu mawili na kwa mara ya kwanza anawaonesha watu Masalia ya Msalaba Mtakatifu. Hata hivyo, hii ni Siku kuu yenye ukuu na maana yake kwani inadhihirisha kuwa Msalaba wa Kristo ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu; ni siku ambayo Msalaba wa Kristo unang’ara duniani! Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu!

Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Waamini watambue ukuu wa Msalaba na wala si tu kama kito cha thamani wanachovaa shingoni au kupamba majumbani mwao, bali ni dira na mwaliko wa kuutafakari upendo wa Yesu aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba iwasaidie waamini kutambua na kuthamini ukuu wa Msalaba, madhara ya dhambi na thamani ya mateso ya Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa watu wote. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya ukimya mkubwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Sala yake wakati wa Njia ya Msalaba, Ijumaa kuu kuzungumza Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2017  alikaza kusema, katika Msalaba wa Kristo, hapo waamini wanawaona watoto wanaoteseka kutokana baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha, lakini kwa bahati mbaya wanakutana na akina Pilato wakiwa wamenawa mikono yao alama kwamba, hawahusiki na jambo lolote! Hapa watu wanakutana na walimu wa sheria, wasiokuwa na huruma, wasiojali maisha wala mahangaiko ya watu; badala ya kufundisha huruma na Injili ya uhai, wanatishia maisha ya watu, kwa adhabu na kifo pamoja na kumhukumu Yesu mwenye haki!

Katika Msalaba waamini wanakutana na viongozi wa Kanisa wasiokuwa waaminifu, badala ya kuuvua utu wao wa kale uliochakaa kama “jani la mgomba” na “kusagika kama kiatu cha raba”, wanaelemewa na mapungufu yao kiasi hata cha kudhalilisha utu na heshima ya watoto wadogo. Kwa njia ya Msalaba, waamini wanawaona mahakimu wanaotoa hukumu ya kifo, ili kuhalalisha matamanio yao binafsi pamoja na kuficha dhambi zao. Katika mateso ya Msalaba, waamini wanaonja vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini, inayotendwa na baadhi ya waamini kwa kuchafua na kulikufuru jina la Mungu, mwingi wa huruma na mapendo.

Katika Fumbo la Msalaba, waamini wanagundua jinsi ambavyo Kanisa linataka kusukumizwa pembezoni mwa jamii kama gari bovu! Na hatimaye, kuondolewa katika maisha ya hadhara, kwa kisingizio cha usawa na uhuru binafsi. Hapa kuna watu wenye uwezo wa kiuchumi wanaojikita katika biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao; ni watu wanaopatia watoto wao fedha inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Msalaba ni kielelezo cha usaliti dhidi ya Yesu kwa vipande thelathini vya fedha; wala rushwa na mafisadi; viongozi waliokengeuka na kukosa maadili; watu wasioguswa na mafao ya wengi! Hapa kuna watu wenye utajiri wa kupindukia wasiojali wala kuguswa na mahangaiko ya maskini kama akina Lazaro wanaoteseka na kufa kwa baa la njaa malangoni pao! Ni watu wanaoharibu mazingira nyumba ya wote kutokana na ubinafsi, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka na kamwe hawajali mafao ya kizazi kijacho! Ni mwelekeo usiowajali wala kuwathamini wazee, wagonjwa na walemavu; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii inayosheheni ubinafsi. Katika Fumbo la Msalaba, waamini wanaliona kaburi la wakimbizi na wahamiaji kwenye kilindi cha Bahari ya Mediterrania huko ambako watu wanazikwa pasi na alama lakini dhamiri za watu zimekufa wala haziguswi na mahangaiko ya watu hawa!

Baba Mtakatifu Francisko katika Sala yake kuhusu Msalaba anaendelea kusema, hiki ni kielelezo cha Fumbo la upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, unaopata hatima yake katika Ufufuko, mfano wa watu wema wanaotekeleza dhamana na majukumu yao bila kutafuta sifa wala kutazamwa na watu wengine! Hiki ni kielelezo cha viongozi waaminifu na waadilifu wanaoshuhudia mwanga wa Kristo Mfufuka kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko; watu wanaojisadaka bila ya kujibakiza. Huu ni mfano bora ya watawa, wasamaria wema walioacha yote ili kuganga na kutibu magonjwa ya umaskini na ukosefu wa haki mintarafu mwanga wa Injili. Hiki ni kielelezo cha watu wenye huruma, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha haki na imani na furaha inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwa kujikita katika utekelezaji wa Amri za Mungu.

Msalaba ni ushuhuda wa wale wanaotubu na kumwongokea Mungu; wanaotambua undani wa madhara ya dhambi zao; watu ambao wako tayari kukimbilia na kuambata huruma ya Yesu Msalabani. Hiki ni kielelezo makini cha watakatifu na wenyeheri wanaong’aa gizani kutokana na imani na matumaini yao hata katika Fumbo la Ukimya wa Kristo! Msalaba ni mfano wa familia zinazoishi kiaminifu ahadi na wito wao wa ndoa. Msalaba ni mfano wa watu wanaojitolea kuwasaidia na kuwahudumia jirani zao bila ya kujibakiza.

Msalaba ni ushuhuda wa wale wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, lakini bado wanathubutu kushuhudia ukweli wa Kristo na Injili yake. Ni mfano wa watu wanaoendelea kukesha ili kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kujikita katika utu na haki. Msalaba ni kielelezo cha Mungu anayependa badala ya kuendekeza chuki na kisasi; Mungu anayependa mwanga badala ya giza ya akili na mioyo ya watu! Msalaba wa Kristo ni nguvu inayomkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti, alama ya Agano Jipya na la Milele, changamoto na mwaliko wa kumtafuta Mungu, mema na mwanga wake wa milele!

Maadhimisho ya Siku kuu ya Kung’ara kwa Msalaba ni nafasi muhimu sana kwa waamini kutafakari: utukufu, ukuu, wema, huruma na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Msalaba uwasaidie waamini kutambua upendo wa Mungu unaowasukuma waamini kuwajibika katika ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Fumbo la Msalaba ni nafasi ya kutafakari ubaya na madhara ya dhambi katika maisha ya watu. Msalaba ni mti wa maisha ya uzima wa milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.