Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko achonga na waandishi wa habari wakati akirejea Vatican

Papa Francisko wakati akirejea mjini Vatican kutoka kwenye hija yake ya kitume nchini Colombia amepata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake.

12/09/2017 09:49

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hija yake ya kitume nchini Colombia iliyokuwa na inaongozwa na kauli mbiu “Demos el primer paso” yaani “Tupige hatua ya kwanza”. Mara tu baada ya kurejea mjini Vatican, Jumatatu tarehe 11 Septemba 2017 majira ya mchana, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, ili kutoa shukrani zake kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi, baada ya kukamilisha hija yake ya kitume iliyomwezesha kutembelea miji minne ya Colombia pamoja na kukutana umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Colombia.

Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya “kuchonga na waandishi wa habari” waliokuwa kwenye msafara wake kwa kuwajibu maswali yao! Kimsingi amegusia kuhusu: amani na upatanisho pamoja ukarimu wa familia ya Mungu nchini Colombia; Dhambi na rushwa; umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi; athari za mabadiliko ya tabianchi; dhamana na wajibu wa kila mtu kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote; maisha na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya. Amekazia umuhimu wa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kuongozwa na kanuni auni.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anayapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anaipongeza Serikali ya Italia na Ugiriki ambazo zimekuwa ni mfano bora sana wa kuigwa katika mchakato wa kuwapokea, kuwahudumia na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowazunguka, licha ya kinzani na magumu yanayoendelea kujitokeza. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kuwa na moyo wa ukarimu kwa kutambua kwamba, hata wao wameonja wema, huruma na ukarimu wa Mungu katika maisha yao.

Jambo la pili katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, anasema, Serikali zinapaswa kujikita katika fadhila ya busara kwa kuangalia rasilimali na miundombinu iliyopo kwa ajili ya kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi kwa kuzingatia utu na heshima yao kama binadamu. Italia imeonesha mfano bora wa kuigwa kwa kuwapatia baadhi ya wahamiaji nafasi ya kujiendeleza katika masomo na huduma za kijamii, hatua kubwa sana. Sera ya huduma kwa wakimbizi ijikite katika busara kama ilivyotumika nchini Sweden. Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote.

Hawa ni watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutoka na vita, ghasia, mipasuko, kinzani pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni watu wanao hatarisha maisha yao huko jangwani na baharini. Inasikitisha kuona kwamba, Bara la Afrika kwa miaka mingi limenyonywa nguvu kazi, rasilimali na utajiri wake. Kuna watu wanaokimbia: vita na njaa; kumbe, kuna haja ya kuliwezesha Bara la Afrika kwa kuwekeza katika shughuli za uzalishaji na huduma, ili watu waweze kupata mahitaji yao msingi. Lakini, kwa bahati mbaya, nchi nyingi zinawekeza Barani Afrika ili kukwapua utajiri na rasilimali za Bara la Afrika.

Baba Mtakatifu anakazia misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba: vurugu na ghasia hazina mashiko katika masuala ya kisiasa kama hali inavyojionesha huko nchini Venezuela. Vatican daima imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, hali ya amani na utulivu inarejea tena nchini Venezuela, lakini hadi sasa mambo yanakwenda kinyume kabisa cha matazamio ya Jumuiya ya Kimataifa. Kinachosikitisha zaidi ni kuona watu wanavyoendelea kupoteza maisha kutokana na njaa na magonjwa pamoja na hali ngumu ya maisha inayowalazimisha wananchi wengi wa Venezuela kuikimbia nchi yao. Umoja wa Mataifa hauna budi pia kuhakikisha kwamba, unatekeleza dhamana na wajibu wake katika kulinda na kudumisha haki msingi za binadanu nchini Venezuela.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni dhamana na wajibu wa kila mtu, lakini wanasiasa na wakuu wa nchi wanayo dhamana ya kimaadili kuhakikisha kwamba, sera na mikakati yao inasaidia kulinda na kudumisha mazingira bora kwa wote. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kujionesha kwa kuwatumbukiza watu katika umaskini mkubwa kama inavyojionesha kwa sasa sehemu mbali mbali za dunia. Wanasayansi wanaonesha dira na mwongozo unaopaswa kutekeleza ili kulinda mazingira. Kumbe, anasema Baba Mtakatifu, kila mtu anao wajibu anaopaswa kuutekeleza kadiri ya hali, nafasi na mazingira yake. Kuna haja ya watu kujipatanisha na Mungu, Jirani na Mazingira, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Uharibifu wa mazingira ni chanzo kikuu cha umaskini na majanga katika maisha ya watu! Utunzaji bora wa mazingira ni kivutio kikuu cha utalii na ukuaji wa uchumi sanjari na maboresho ya maisha ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapenda kuwajengea vijana wa kizazi kipya imani, matumaini na mapendo katika maisha yao, ili waweze kuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi machungu katika maisha! Vijana wanapaswa kuwa makini ili wajanja wachache wasiwapokonye furaha na matumaini yao kwa siku za usoni kwa kuwatumbukiza katika mifumo ya utumwa mamboleo na ghasia, mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima yao kama binadamu. Kuna haja kwa wanasiasa, watunga sera na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakihakikisha kwamba, wanajitahidi kuunganisha, kulinda na  kudumisha umoja na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana watambue na kuthamini asili yao, bila ya kuwa na mizizi thabiti, vijana wengi watapokwa matumaini kwa siku za usoni!

Baba Mtakatifu akiendelea kuchonga na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake anasema, anapenda kuishukuru familia ya Mungu nchini Colombia kwa wema, ukarimu na upendo waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume; kwa kujipanga kwenye barabara, kuwatoa watoto wao ili aweze kuwabariki na kwamba, hii ni hazina na amana ya matumaini ambayo anaendelea kuihifadhi katika sakafu ya moyo wake.  Baada ya kupiga hatua ya kwanza, sasa wananchi wa Colombia hawana budi kupiga hatua ya pili inavyovuka vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa muda wa miaka 54, kwa kujikita katika amani, upatanisho, umoja na mshikamano wa kitaifa. Wananchi waondokane na kishawishi cha rushwa na ufisadi wa mali ya umma kwani hii ni dhambi kubwa inayomjenga mtu kiburi cha kutoona kwamba, anahitaji huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawaombea wala rushwa na mafisadi ili waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

12/09/2017 09:49