Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Mradi wa makazi ya watu wa Talitha Kum ni faraja ya maskini

Papa Francisko akiwa Jimbo kuu la Cartagena amebariki jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya watu maskini, ili kuwajengea matumaini ya maisha yaliyo bora zaidi.

11/09/2017 13:29

Baba Mtakatifu Francisko, katika hija yake ya kitume nchini Colombia, Jumapili, tarehe 10 Septemba 2017, ametembelea Jimbo kuu la Cartagena, akiwa anaongozwa na kauli mbiu “Utu wa binadamu na haki msingi za binadamu”. Amebariki jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watu wasiokuwa na makazi maalum inayosimamiwa na kuendeshwa na Chama cha Kitume cha Talitha Kum, maana yake katika Maandiko Matakatifu ni “Msichana, nakuambia, inuka”. Kwa muda wa miaka minne sasa kituo hiki ni sehemu ya utume wa Jimbo kuu la Cartagena.

Itakumbukwa kwamba, Chama hiki kilianzishwa kunako mwaka 1835, ili kutoa msaada kwa maskini na wahitaji zaidi. Chama hiki kinashirikiana kwa karibu zaidi na Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kimataifa unaojulikana pia kama “Talitha Kum” kwa ajili ya mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo ambayo yanaendelea kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kituo hiki cha Talitha Kum, kimekuwa ni msaada wa pekee sana kwa wasichana zaidi ya 70 wanaopewa huduma katika vyuo vikuu mjini Cartagena, ili kuboresha matumaini ya maisha yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Ujenzi wa kituo kipya, ambao jiwe lake la msingi limebarikiwa na Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Colombia kinapania kuwahudumia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi wapatao mia 500 hadi 600. Hili ni tukio ambalo limeshuhudiwa na maskini pamoja na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu pia amepata nafasi ya kumtembelea Mama Lorenza, mwenye  umri wa miaka 77 ambaye amekuwa akijisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watu maskini kwa muda wa miaka 50. Baba Mtakatifu Francisko akiwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro Claver, amebariki Jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha Chama cha Kitume cha Talitha Kum. Baba Mtakatifu katika sala hii, amemshukuru Mwenyezi Mungu aliyewakirimia wanadamu Injili na Amri ya Upendo, ili aweze kuwapatia baraka watumishi wake wanaotaka kujizatiti kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao! Kwa njia yake, waweze kuwahudumia jirani zao kwa ari na moyo mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

11/09/2017 13:29