2017-09-10 15:25:00

Jilindeni na vishawishi vya dunia hii kwa sala na unyenyekevu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 9 Septemba 2017 baada ya kuhitimisha utume wake mjini Medellìn ambako aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa familia ya Mungu, akatembelea nyumba ya Mtakatifu Yosefu na hatimaye kuzingumza na wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wazazi wao alirejea tena mjini Bogotà na kukutana na mapadre, watawa na watu wa ndoa waliokuwa wanaadhimisha Jubilei zao. Baba Mtakatifu Francisko akiwa kwenye Ubalozi wa Vatican, amekumbushia wito wa Mtakatifu Petro aliyeteuliwa kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa lake. Lakini, hata hivyo kila mwamini ameteuliwa na Kristo kushiriki katika ujenzi wa Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa.

Mtume Petro alifurahi sana alipoambiwa na Kristo kwamba, yeye ni mwamba na juu ya mwamba huu, Kristo alitaka kulijenga Kanisa lake! Petro mtume, akaingiwa na kiburi na udhaifu wa binadamu na kusahau mpango wa Mungu katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kiasi cha kumkataza kwamba, kamwe Fumbo la Msalaba halitamkuta! Lakini, Yesu akamkea na kumwambia kuwa ni shetani na alipaswa kurudi nyuma na kuanza kujifunza tena! Petro anakumbuka siku ile alipomsaliti Yesu kwa kumkana mara tatu kwamba, hamfahamu hata kidogo! Yesu alipofufuka kwa wafu na kukutana na wanafunzi wake, waliokuwa wamekata tamaa na kurejea tena katika shughuli zao za uvuvi kwa shida kubwa! Alimuuliza Petro mtume, ikiwa kama kweli alikuwa anampenda kuliko Mitume wengine wote!

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, wito wa kwanza unafumbatwa katika upendo wa Kristo, changamoto kwa waamini kukumbuka siku ile ya kwanza walipokutana na Kristo katika maisha yao! Katika safari ya maisha, wamekuwa na nyakati za furaha, matumaini na majonzi moyoni. Yesu amempatia kila mwamini jina ambalo anapaswa kuliendeleza katika maisha na utume wake. Wakati mwingine, majina haya yanabadilika kadiri ya nafasi na mazingira. Kumbe, wanapaswa kujilinda wao wenyewe kwa njia ya sala, unyenyekevu pamoja na kujiaminisha kwa Kristo Yesu, ili waweze kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao katika Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wawe wadumifu katika kuliendeleza jina lao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia ukuu wa Mungu unaojifunua katika historia ya wokovu. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru mapadre, watawa na waamini wote waliofika kushuhudua matendo makuu ya Mungu katika maisha yao! Wote hawa amewapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.