2017-09-09 16:21:00

Yaliyojiri kwenye Ibada ya Upatanisho wa Kitaifa nchini Colombia


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican katika makala haya maalum inapenda kukuletea kwa muhtasari yale yaliyojiri kabla na baada ya maadhimisho ya Liturujia ya Upatanisho wa Kitaifa nchini Colombia. Mshikamano wa Baba Mtakatifu Francisko na waathirika wa majanga asilia huko Amerika ya Kati na Ukanda mzima wa Caribbean. Amegusia umuhimu wa kuwaheshimu na kuwathamini walemavu kwani hii ni sehemu ya udhaifu wa binadamu unaopaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kupatiwa tiba muafaka pale inapowezekana. Papa Francisko anawataka wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kujisadaka zaidi kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha amani na utulivu kati ya watu!

Katika maadhimisho ya Liturujia ya Upatanisho wa Kitaifa nchini Colombia kama kilele cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia, Ijumaa, tarehe 8 Septemba 2017 amesikiliza kwa umakini mkubwa shuhuda zilizotolewa na waathirika wa vita, ghasia na mipasuko ya kijamii nchini Colombia kwa takribani miaka 50 iliyopita! Baba Mtakatifu anasema, hii si siku ya kutoa hotuba wala mahubiri, bali anamwomba Mwenyezi Mungu amkirimie neema ya kuweza kuwakumbatia wote na kuwahifadhi katika sakafu ya moyo wake; neema ya kuweza kulia, kusali na kuanza mchakato wa msamaha wa kweli unaobubujika kutoka katika Imani na matumaini, tayari kupiga moyo konde na kusonga mbele!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tangu mwanzo wa hija yake ya kitume, ametamani sana siku hii ya upatanisho wa kitaifa, ambayo imemwezesha kukutana na wananchi wa Colombia ambao ndani mwao wanabeba mambo mazito ya historia inayofumbata majanga ya maisha ya binadamu! Lakini, hii pia ni historia inayojikita katika matukio ya kishujaa yanayoashiria tunu msingi za maisha ya kiroho na matumaini thabiti. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, yuko kati yao kama Musa aliyekuwa anatembea katika ardhi takatifu, ambayo imelowanishwa kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia; mateso na mahangaiko ya ndugu, jamaa na marafiki wa wale wote waliokuwawa kikatili, waliopotea katika mazingira ya kutatanisha au watu waliolazimika kuikimbia nchi yao kutokana na vita, ghasia na machafuko ya kijamii!

Colombia ni nchi ambayo bado ina madonda mabichi kabisa yanayochuruzika damu, kwani kila vita, ghasia na mauaji ni mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu;  na kwamba, kila mauaji yaliyotokea yamekwenda kinyume cha utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wamekutanika chini ya Msalaba wa Bojaya, ambako tarehe 2 Mei 2002, mauaji ya kinyama yalitendeka dhidi ya watu waliokuwa wamekimbilia kupata hifadhi ndani ya Kanisa, kielelezo cha: mauti, mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia.

Baba Mtakatifu anasema, kumwona Kristo Msalabani akiwa hana mikono wala miguu, bali uso wake wenye huruma, ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kina. Huu ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na watu wake; Kristo anayeteseka na kuonya kwamba, chuki na uhasama si hatima ya maisha ya binadamu, kumbe, kuna haja ya kugeuza mateso na mahangaiko ya ndani kuwa ni chemchemi ya maisha na ufufuko, ili kwa njia pamoja na Kristo Yesu, watu waweze kujifunza nguvu ya msamaha na ukuu wa upendo usiokuwa na mipaka!

Baba Mtakatifu amewashukuru mashuhuda wa athari ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii nchini Colombia walioshirikisha historia ya mateso, upendo, msamaha na maisha yenye matumaini yanayowasukuma kugeuza kisogo dhidi ya chuki na uhasama; hali ya kutaka kupiliza kisasi na machungu ya moyoni! Hawa ni mashuhuda ambao wanaonesha kwamba, fadhili na kweli zimekutana; haki na amani zimebusiana, kielelezo cha moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu na moyo mkuu unaotafuta msamaha, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa amani na utulivu nchini Colombia.

Pastora Mira kwa upande wa ushuhuda wake ameomba: baraka na neema ya msamaha ili kuondokana na mzunguko wa kifo kwani kwa msaada wa Kristo Yesu, yote yanawezekana kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya uhai. Msalaba wa Bojaya, umekuwa kweli ni chemchemi msamaha na upendo; matumaini na amani kwa familia ya Mungu nchini Colombia, dhidi ya utamaduni wa kifo! Luz Dary kwa upande wake, amekaza kusema, si rahisi sana kuganga na kuponya madonda ya ndani, lakini kwa neema na huruma ya Mungu inawezekana kuwa shuhuda wa upendo unaokoa na kujenga, mwanzo wa mchakato wa kuganga na kuponya madonda yaliyojeruhi utu na heshima ya binadamu, tayari kuwasaidia watu wengine wanaoteseka: kiroho na kimwili! Watu wanahitaji “kutembelea magongo ya upendo na msamaha” katika maisha yao!

Baba Mtakatifu amewashukuru Deisy na Juan Carlos walioshuhudia kwamba, walau wananchi wote wa Colombia wameathirika kutokana na vita hii. Ni jukumu na dhamana ya vijana kujibidisha katika masomo na maadili mema, ili wasitumbukie katika: vita, ghasia na mtandao wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya! Hata wale waliotenda ubaya, wanayo nafasi ya kutubu na kuongoka, utume uliotekelezwa na Kristo Yesu, ili waweze kupyaishwa tena kimaadili na katika maisha ya kiroho, ili kweli haki iweze kukita mizizi yake katika maisha ya watu! Huu ndio mchango unaopaswa kutolewa na kila mwananchi wa Colombia kwa kuhakikisha kwamba, anachangia kwa hali na mali katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya vita, ghasia, chuki na uhasama kati ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema si rahisi sana kukubali mabadiliko katika maisha kwa watu ambao wametumia vita, ghasia na mipasuko ya kijamii kwa ajili ya mafao yao binafsi; watu waliojitajirisha kwa njia za ulaghai kwa kudhani kwamba, walikuwa wanasaidia kulinda maisha ya ndugu na jirani zao. Kila mtu anaweza kupiga hatua ya amani na upatanisho, lakini, ikumbukwe kwamba, bado kuna “magugu” nchini Colombia. Jumuiya inayojiinjilisha daima inajali matunda, kwani Mwenyezi Mungu anaitaka izae matunda. Inajali juu ya mbegu na haipotezi subira kwa sababu ya magugu. Mpanzi anaruhusu magugu na ngano vikue pamoja ili kuzaa matunda ya uhai mpya, hata kama kwa kiasi fulani yanaonekana kuwa na mapungufu fulani.

Baba Mtakatifu anasema, hata katika vita, ghasia na machafuko, bado haki na huruma vitakumbatiana na kubusiana na hivyo kumwilisha historia nzima ya wananchi wa Colombia. Kumbe, huu ni wakati wa kuganga na kuponya machungu ya moyo na kumkaribisha kila mtu aliyetenda makosa haya ili aweze kujitambua, kutubu na kujikita Zaidi katika kurekebisha hali ya maisha  kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii mpya inayong’arishwa kwa haki na amani. Huu ndio ushuhuda makini uliotolewa na Juan Carlos anayekiri kuhusu umuhimu wa mchakato wa amani na upatanisho ambao kimsingi ni mrefu na mgumu, lakini umesheheni matumaini na upatanisho, changamoto na mwaliko kwa kupokea na kukubali ukweli! Hii ni changamoto pevu, lakini muhimu sana, kwani ukweli ni mwandani wa haki na huruma nyenzo msingi katika ujenzi wa amani. Ukweli uwawezeshe watu kufikia upatanisho na msamaha na wala si kuchochea tabia na hali ya kulipizana kisasi. Ukweli usaidie kufafanua yale yaliyowatokea ndugu zao waliopotea katika mazingira ya kutatanisha. Ukweli wapatie ujasiri wahusika kutubu mateso na suluba walizowatendea watoto wadogo kwa kuwapeleka mstari wa mbele kwenye mapambano. Ukweli utambue kashfa na aibu ya nyanyaso walizowatendea wanawake.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa tafakari hii ya kina anapenda kuwaalika watu wa Mungu nchini Colombia kufungua mioyo yao ili kujipatanisha na Mungu! Wasiogope ukweli na haki; kupokea na kutoa msamaha; kujipatanisha na wale wanaopiga hatua ya kwanza kwa kufanya toba na kuomba msamaha, ili kujenga udugu na urafiki kati ya watu. Huu ni muda wa kuganga na kuponya madonda; kujenga madaraja na kubomoa kuta za utengano na hali ya kutojali! Ni muda wa kuzima tabia ya kulipiza kisasi na kuanza kuwasha moto wa haki, utulivu, ukweli na udugu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anawataka wananchi wote wa Colombia kuwa ni wajenzi wa amani mahali penye vita, vurugu na ghasia; wawe kweli ni mashuhuda upendo na huruma.

Baba Mtakatifu Francisko mbele ya Msalaba wa Boyaja amewakumbusha waamini mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani; amewaonesha upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Yesu Mteswa na kwamba, mbele yao wanayo dhamana na wajibu wa kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo; kwa kuwasaidia maskini; kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kubariki na kufariki wale wanaolia na kuteseka katika hali ya upweke, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo usiokuwa na mipaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.