2017-09-09 16:04:00

Papa Francisko: wanajeshi lindeni na kudumisha amani na usalama!


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 8 Septemba 2017 akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bogotà, kuelekea Jimbo kuu la Villavicencio, nchini Colombia katika hija yake ya kitume, amewatangaza watumishi wa Mungu Askofu Jesús Emilio Jaramillo Monsalve wa Jimbo Katoliki la Arauca, na Padre Pedro María Ramírez Ramos kuwa wenyeheri pamoja na kuadhimisha Liturujia ya Upatanisho wa Kitaifa nchini Colombia, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na wahudumu wao wa maisha ya kiroho nchini Colombia.

Baba Mtakatifu amewashukuru kwa sadaka na majitoleo yao katika kudumisha ulinzi na usalama kwa watu na mali zao; amani na utulivu wakati huu wa hija yake ya kitume nchini Colombia kwani uwepo wake unawapatia kazi ya ziada. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kujibidisha katika kukuza na kudumisha haki, amani na utulivu na hata wakati mwingine, wamethubutu hata kuhatarisha maisha yao. Hivi ndivyo alivyofanya Kristo Yesu kwa kuwapatanisha watu na Baba yake wa mbinguni kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Baba Mtakatifu anawataka wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kuthubutu kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha amani.

Baba Mtakatifu anawataka waendelee kujizatiti katika mchakato wa amani na upatanisho, jambo muhimu sana linalogusa maisha ya wananchi wa Colombia. Baba Mtakatifu aliwaalika wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliopoteza maisha yao wakiwa katika utume wao kama Askari; wamewaombea waliopata ulemavu wakiwa kazini, ambao pia waliwakilishwa uwanjani hapo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.