Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko asikitishwa na maafa makubwa ya majanga asilia!

Papa Francisko amesikitishwa sana na madhara makubwa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi nchini Mexico pamoja na tufani ya Irma kwenye Ukanda wa Caribbean. - AFP

09/09/2017 14:34

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria, tarehe 8 Septemba 2017 akiwa Jimbo kuu la Villavicencio, nchini Colombia katika hija yake ya kitume, amewatangaza watumishi wa Mungu Askofu Jesús Emilio Jaramillo Monsalve wa Jimbo Katoliki la Arauca, na Padre Pedro María Ramírez Ramos kuwa wenyeheri. Amesema, wenyeheri hawa wapya ni wafiadini kutoka Armero, alama ya watu wa Mungu wanaotaka kutoka katika mnyororo wa vita, ghasia na mateso moyoni. Mada kuu iliyokuwa inaongoza, maadhimisho huko Villavicencio ni “Kujipatanisha na Mungu, Wacolombiani pamoja na mazingira”.

Baba Mtakatifu mara tu baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu, alimshukuru kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Óscar Urbina Ortega, wa Jimbo kuu la Villavicencio na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuonesha uwepo wa karibu kwa njia ya sala kwa wale wote walioathirika la tetemeko la ardhi ambalo hivi karibuni limeikumba nchi ya Mexico na hivyo kusabababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikisha wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya uwepo wake wa karibu; anapenda kuwafariji wale waliondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao. Taarifa zinaonesha kwamba, watu 61 tayari wamekwisha kufariki dunia na miji iliyoathirika sana ni Oaxaca na Chiapas, huko Mexico Hili ni tetemeko kubwa kuwahi kutoka nchini Mexico katika kipindi cha miaka 85 iliyopita!

Baba Mtakatifu anasema, anafuatilia kwa karibu zaidi mwenendo wa “Tufani ya Irma” ambayo inaendelea kusababisha maafa makubwa  katika Ukanda wa Caribbean. Hadi sasa kuna watu kadhaa wamekwisha kufariki dunia pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na makazi ya watu; hali ambayo imesababisha watu wengi kujikuta hawana makazi. Baba Mtakatifu anasema, wote hawa anawabeba katika sakafu ya moyo wake, kwa njia ya sala na hivyo anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye kwa ajili ya kuwaombea watu wote hawa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

09/09/2017 14:34