Baba Mtakatifu Francisko ametuma salamu zake za rambi rambi kutokana na kifo cha
Kardinali Carlo Caffarra, askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Bologna aliye kuwa na
umri wa miaka 79. Kifo cha Kardinali Carlo Caffarra kilitokea tarehe 6 Septemba Jimboni
Bologna nchini Italia.
Kufuatiwa na kifo hicho, telegram ya Baba Mtakafu kupitia kwa Askofu Mkuu Matteo
Zuppi wa Jimbo Kuu la Bologna anaonesha masikitiko yake na kushiriki uchungu na Jumuiya
nzima ya Jimbo la Bologna na familia yake kuondokewa na mpendwa wao na Kanisa zima.
Akikumbuka maisha yake Kardinali Carlo Caffara, Baba Mtakatifu anaeleza juu ya huduma yake ya kichungaji kwamba, aliitenda kwa uamninifu, furaha na upendo wa kina kwa Kanisa. Ameonesha juhudi yake pamoja na ukarimu wake wa kitume hasa akiwa mstari wa mbele, mwanzilishi na profesa wa Chuo cha Kipapa cha Yohane Paulo II, katika mafunzo ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anaongeza, Kardinali Carlo amejikita sana katika shughuli ya kitume bila kuchoka na kupenda sana Kanisa katika majimbo makuu ya Ferrara na Comacchio na baadaye kama kiongozi mwenye hekima na msimamo wa kuongoza majimbo makuu.
Mwisho Baba Mtakatifu anatoa maombi yake kwa njia ya Bikira Maria na Mtakatifu
Petroni msimamizi wa Jimbo la Bologna ili Bwana apokee roho ya mwaamini na mtumishi
wake kwenye kiti cha enzi hukoYerusalemu mpya.
Mazishi ya Kardinali Carlo Caffarra yatafanyika Jumamosi 9 Septemba saa tano asubuhi
katika Kanisa Kuu Bologna nchini Italia.
Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
All the contents on this site are copyrighted ©. |