2017-09-08 12:10:00

Papa Francisko: Tangazeni ni kushuhudia furaha ya Injili katika utume


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia, Alhamisi, tarehe 7 Septemba 2017 amekutana pia na Kamati kuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM; kwa kukazia umuhimu wa kujikita katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika maisha na utume wa Kanisa; kutangaza kweli za Kiinjili, kulinda amana ya Mkutano wa Aparecida; umuhimu wa vijana Amerika ya Kusini; dhamana na utume wa waamini walei na kwamba, wanapaswa kuwa na ari na mwamko wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mkutano mkuu wa Aparecida ni amana na utajiri mkubwa kwa Kanisa la Amerika ya Kusini! Kumbe, kuna haja ya kujifunza mbinu mkakati wake unaojikita katika ushirikishwaji wa Makanisa Mahalia katika maisha na utume wa Kanisa huko Amerika ya Kusini. Utume wa Yesu unapaswa kuwa ni kiini cha maisha na mikakati yote ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Makanisa Mahalia. Kwa namna ya pekee, wainjilishaji wanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha kwa watu wanaoinjilishwa.

Wakleri wakumbuke daima kwamba, wao ni wachungaji na wainjilishaji na wala si watu wa mshahara, kumbe, wanapaswa kutoa ujumbe unaogusa sakafu ya mioyo ya watu wao kama afanyavyo Baba mwenye huruma. Wajizatiti kikamilifu katika Injili ya Kristo kwa kukazia utume wa kimisionari, tayari kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa. Wawe tayari kumuiga Kristo Yesu aliyekuwa karibu sana na watu, akajenga madaraja ya kuwaunganisha watu mbali mbali, mtindo wa maisha ambao hata Wakleri wanaweza kuumwilisha katika maisha na utume wao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni rahisi sana kuadhimisha tukio la Imani ndani ya Kanisa kwa kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 ya Medellìn, Miaka 10 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Kichungaji “Ecclesia in America” yaani “Kanisa Barani Amerika” na Miaka 10 ya Mkutano wa Aparecida. Haya ni matukio ambayo yanapasa kulisadia Kanisa Amerika ya Kusini kulinda na kudumisha amana na utajiri wake, kwa kuimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu ili kudumisha utume wa Kanisa Amerika ya Kusini katika umoja! Wainjilishaji wajifunze mfumo na mtindo wa maisha ya Yesu aliyejitahidi kutembea ili kukutana na watu katika uhalisia wa maisha yao: akawaganga na kuwaponya, akawasikiliza na kuwaokoa! Utume wa Kanisa unatekelezwa kwa kuzingatia hali halisi ya maisha ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, inasikitisha sana kuona watu wengi Amerika ya Kusini wamekata tamaa ya maisha na baadhi ya watu wanatumia mwanya huu kwa ajili ya kujitajirisha. Familia ya Mungu Amerika ya Kusini ina utajiri mkubwa sana wa maisha ya kiroho, kumbe, inapaswa kusaidiwa ili kung’amua maana na uwepo wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Kuna mamilioni ya vijana Amerika ya Kusini ambayo hayana matumaini; kati yao kuna wale ambao wameathirika na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya! Kanisa halina budi kuwekeza rasilimali muda na fedha katika ulimwengu wa vijana wa kizazi kipya ili kuwaonesha njia inayowapeleka kwa Mwenyezi Mungu, ili kweli vijana hawa waweze kuwa ni wadau wakuu katika maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini.

Baba Mtakatifu anawahimiza waamini walei kutambua na kuthamini dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa. Walei watekeleze dhamana na wajibu wao katika hali ya utulivu, kwa kuwajibika, kwa kuonesha weledi, mwelekeo mpana na umakini. Waamini walei wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi, kwani matumaini ya familia ya Mungu Amerika ya Kusini yanaritishwa kwa njia ya waamini walei. Mwishoni, Baba Mtakatifu analitaka Kanisa Amerika ya Kusini kuwa shuhuda na chombo cha uinjilishaji, kwa kutembea bega kwa began a watu wa Mungu majimboni mwao kama alivyofanya Mtakatifu Toribius Alfonso wa Mogroveio aliyetumia miaka 18 kati ya miaka 24 ya utume wake kama Askofu katika vijiji vya Jimbo lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.