Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Colombia jipatanisheni na Mungu, Jirani na Mazingira!

Papa Francisko anawataka wananchi wa Colombia kujipatanisha na Mungu, Jirani na Mazingira! - AFP

08/09/2017 15:59

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria, tarehe 8 Septemba 2017 akiwa Jimboni Villavicencio, Colombia katika hija yake ya kitume, amewatangaza watumishi wa Mungu Askofu Jesús Emilio Jaramillo Monsalve wa Jimbo Katoliki la Arauca, na Padre Pedro María Ramírez Ramos kuwa wenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu iliyosheheni umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Colombia! Wenyeheri hawa wapya ni wafiadini kutoka Armero, alama ya watu wanaotaka kutoka katika mnyororo wa vita, ghasia na mateso moyoni. Mada kuu iliyokuwa inaongoza, maadhimisho huko Villavicencio ni “Kujipatanisha na Mungu, Wacolombiani pamoja na mazingira”.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ameelezea kwa ufupi maisha na utume wa Bikira Maria aliyezaa Jua la haki linaloangaza walimwengu. Injili imesimulia muhtasari wa historia ya watu wa Mungu inayofumbatwa katika maisha ya utakatifu na dhambi, lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo akaonesha kwamba, wokovu unafumbatwa katika uhalisia wa maisha ya watu na kwamba, waamini wote ni sehemu ya historia hii kubwa ya watu wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao yote yanayoweza kufananishwa na maisha ya uhamishoni. Mwinjili Mathayo katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu anawataja wanawake walioshiriki kikamilifu katika kutekeleza mpango wa wokovu uliokuwa umenuiwa na Mwenyezi Mungu tangu awali! Mpango huu unatekelezwa katika Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, kutokana na utayari wa Bikira Maria kukubali mpango wa Mungu katika maisha yake! Mtakatifu Yosefu anaoneshwa kuwa ni mtu wa haki, mwenye heshima na huruma, aliyesaidiwa na kuangazwa na Mwenyezi Mungu hata kukubali kufanya maamuzi mazito katika maisha yake!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, familia ya Mungu nchini Colombia ni sehemu ya watu wa Mungu, wenye historia, upendo na mwanga anngavu ambayo, wakati mwingine imetembea katika giza, vita, ghasia na kifo. Wamejikuta wakiwa uhamishoni na bondeni kwenye machozi! Kuna watu waliojitahidi kutafuta mafao ya wananchi wa Colombia kwa kufungamanisha haki na wema, ili kuwezesha mwanga wa mchakato wa upatanisho kushika kasi! Hii ni changamoto ya kuweka kando kiburi na kuanza kukumbatia ukweli wema na upatanisho! Yote haya yanawezekana ikiwa kama wananchi wa Colombia wataweza kuruhusu mwanga wa Injili uweze kupenya katika historia ya dhambi, ghasia na kinzani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, upatanisho ni mlango unaowafungulia watu wote walioathirika kwa vita na ghasia ili kushinda kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi na kujichukulia sheria mkononi na kwa njia hii, wanakuwa ni wahusika wakuu katika mchakato wa ujenzi wa amani na upatanisho. Watu wenye imani na matumaini thabiti wanaweza kuthubutu kuanza kupiga hatua katika mwelekeo huu kwa kutambua madhara ya kinzani na hatimaye, kuamua kupiga moyo konde na kuanza safari ya kukutana na ndugu ili kuvuka kishawishi cha ubinafsi, maamuzi mbele na hatimaye, kujivika ukarimu na utu wema ili kujenga mshikamano na mafungamano ya kijamii yanayojikita katika utu na heshima ya binadamu wote.

Mchakato wa upatanisho ni kazi na matunda ya wananchi wote wanaotamani kujenga kesho yenye matumaini. Jitihada zote hizi pasi na utekelezaji makini wa amani, upatanisho itabaki ni dhana inayoelea kwenye ombwe! Baba Mtakatifu amewataka wananchi wa Colombia kujipatanisha na mazingira nyumba ya wote! Mazingira yanalia na kutoa damu kutokana na ukatili uliojikita katika sakafu ya moyo wa binadamu ambao umejeruhiwa na dhambi ya asili. Matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa mazingira. Sasa ni wajibu wa wananchi wote wa Colombia kujizatiti katika kulinda na kutunza mazingira kama kielelezo makini cha upatanisho wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

08/09/2017 15:59