2017-09-08 11:52:00

Papa Francisko asema, mchakato wa amani na upatanisho ni muhimu sana!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kukutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Colombia, Alhamisi, tarehe 7 Septemba 2017 alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia na kukazia umuhimu wa kuwa na ujasiri wa kupambana na kifo, ili kuwatangazia watu wa Mungu nchini Colombia ushindi wa Ufufuko wa Kristo! Waoneshe upendo kwa waamini wao bila ubaguzi; wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa  upatanisho wa kitaifa, tayari kuendeleza utume na dhamana ya Mama Kanisa nchini Colombia sanjari na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu amewaambia Maaskofu wa Colombia kwamba, wao ni muhimu sana katika kupiga hatua ya amani ya kweli, upatanisho; kwa kukataa ghasia na vurugu kama njia ya kupambana na maisha; wajitahidi kubomoa kuta za ukosefu wa usawa ambao kimsingi ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya wananchi wengi wa Colombia. Wajizatiti kikamilifu kupambana na rushwa pamoja na ufisadi, daima wakijitahidi kusimama kidete kudumisha maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amewakumbusha Maaskofu wa Colombia kwamba, mchakato wa amani na upatanisho nchini mwao ni jambo la pekee kabisa linalofumbata utajiri wa kiutu ambao chimbuko lake ni imani inayowasukuma kupambana na utamaduni wa kifo unaotangazwa na hata wakati mwingine kupandikizwa miongoni mwa watu! Maaskofu wawe na ujasiri wa kukiona kifo machoni pao, tayari kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II walipiga hatua ya kwanza katika mchakato wa amani na upatanisho, lakini ikumbukwe kwamba, ni Mwenyezi Mungu anayepiga hatua ya kwanza kabisa kama alivyofanya kwa Abrahamu, Baba wa Imani, Musa, Nabii wa Mungu na hatimaye katika Fumbo la Umwilisho, daima akionesha dira na njia ya kufuata! Maaskofu wajitahidi kuwa huru kwa kudumisha mahusiano yao na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Sakramenti na Tafakari ya Neno la Mungu tayari kumwilisha mambo yote haya katika maisha na utume kwa Kristo Yesu aliyewateua na kuwatuma shambani mwake!

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu wa Colombia kuhakikisha kwamba, wanatunza na kudumisha umoja na utofauti unaojitokeza miongoni mwao; kwa kuwa makini katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; historia na utajiri wa mang’amuzi ya maisha ya Kikanisa. Wawe ni wajenzi wa Kanisa linalotoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko nchini Colombia, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni la wote na wala si kwa ajili ya watu wachache peke yao! Wathamini uwepo wa wananchi wa Colombia wenye asili ya Kiafrika. Maaskofu wawe mstari wa mbele kugusa madonda ya historia na wananchi wa Colombia kwa kutambua kwamba, wao ni wachungaji na wala si wanasiasa wala wataalamu, kumbe, dhamana na wajibu wao ni kutangaza na kushuhudia: uhuru, upatanisho na huruma ya Mungu; daima wakiwa tayari kuwatafuta na kuwahudumia ndugu zao na kamwe wasitumbukie kwenye kishawishi cha kuomba wala kupokea rushwa inayoweza kuwanyima uhuru wa maisha na utume wao kama viongozi wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu wa Colombia kujikita katika huduma makini ya binadamu: kiroho na kimwili, katika hali ya amani na utulivu! Wasimame kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Wajizatiti kupambana na ghasia, balaa ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia, mambo yanayofifisha ndoto ya vijana wa kizazi kipya. Vijana waambiwe kwamba, inawezekana kupata mafanikio pasi na kujitumbukiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya na kwamba, kanuni maadili na utu wema ni silaha madhubuti katika ukomavu wa mtu: kiroho na kimwili.

Rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni mambo hatari katika mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuwa karibu Zaidi na wakleri pamoja na watawa wao, kwa kuwapatia majiundo makini ya awali na endelevu sanjari na kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao msingi, vinginevyo, wanaweza kujikuta wakimezwa sana na malimwengu! Mwishoni, Baba Mtakatifu analiaminisha Kanisa nchini Colombia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu wa Chiquinquirà. Kila mmoja wao, ajitafiti mwenyewe na kuangalia ikiwa kama kweli anatembea katika njia haki kwa kulinda na kudumisha ile zawadi waliyoipokea bure kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa liwe ni mdau mkubwa wa utunzaji bora wa mazingira ya Amazzonia kwani uchafuzi mkubwa wa mazingira una athari zake kwa maisha ya watu: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.