2017-09-08 11:12:00

Papa Francisko anawataka vijana kuwa ni vyombo vya haki na amani!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia, Alhamisi, tarehe 7 Septemba, 2017 alipata nafasi ya kumtembelea Rais Juan Manuel Santos Calderon wa Colombia na hivyo kubadilishana zawadi. Baadaye, alitembelea Kanisa kuu la Jimbo kuu la Bogotà na kusalimiana na waamini waliokuwepo Kanisani hapo. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewaombea amani wananchi wa Colombia na kwamba, yuko kati pamoja nao kama hujaji wa amani na matumaini na kwamba, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake kwa familia ya Mungu nchini Colombia.

Baba Mtakatifu anasema, amekuja ili kujifunza kutoka kwao imani thabiti iliyowawezesha kupambana na vyema na kinzani za maisha na kwamba, Mwenyezi Mungu yuko daima pamoja nao, bila ubaguzi kwa mtu awaye yote! Akiwa kati yao, anapenda kuwashirikisha siri kuu kwamba, kweli wanapendwa sana na Mwenyezi Mungu na anataka kuwatia shime ili waweze kusonga mbele wakitafuta na kutamani amani ya kweli na inayodumu. Amewashukuru vijana kutoka sehemu mbali mbali za Colombia waliofika kumpokea na kwamba, vijana kwake ni chemchemi ya furaha, ambayo kamwe hakuna mtu anayeweza kuwapokonya.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuirutubisha furaha iliyomo ndani mwao kwani inafumbatwa katika upendo kwa Mungu na jirani; tayari kuleta mabadiliko katika jamii, ili kutimiza ndoto zinazofichika katika sakafu ya mioyo yao! Baba Mtakatifu anawataka vijana kupiga moyo konde na kamwe wasiwe na wasi wasi ya kesho, bali wathubutu kuota ndoto ya kutambua mateso na mahangaiko ya jirani zao; wawe tayari kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao; hata katika shida, mateso na mahangaiko yao ya ndani, vijana wawe na ujasiri wa kuwasaidia wazee na kamwe wasikubali kujenga mazoea ya kubaki katika mateso makali na hali ya kukata na kujikatia tamaa.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutambua shida na mahangaiko ya jirani zao si kwa ajili ya kutoa hukumu na kuwanyooshea watu wengine vidole, bali wawe na ujasiri wa kutambua makosa hali ambayo pengine, vijana wengine hawakupata bahati na nafasi kama hii. Colombia inawahitaji sana vijana ili kuiboresha na kuipyaisha, ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Vijana watambue kwamba, wanao wepesi wa kukutana na wengine katika medani mbali mbali za maisha, kumbe, wanaweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa utamaduni wa kukutana na watu, licha ya tofauti zao mbali mbali, bali wote kwa pamoja wanaunda familia ya Mungu nchini Colombia.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa kweli ni vyombo vya upatanisho; kwa kuondokana na chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipiza kisasi na badala yake, kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu! Mbele yao wanayo changamoto ya kuganga na kuponya madonda ya kinzani na mipasuko ya kijamii; mambo ambayo yanawanyima vijana matumaini! Wawe ni vyombo vya matumaini ili kuleta mwamko mpya nchini Colombia! Wawe na ujasiri wa kugundua utajiri unaofumbatwa katika rasimali za nchi, tamaduni na maisha ya watu wake, tayari kuvalia njuga changamoto hii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Colombia.

Vijana wawe mstari wa mbele katika ujenzi wa nchi yao, kwa kutambua kwamba, wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vijana wanapaswa kuwa ni wajumbe wa amani na matumaini na kamwe wasikubali “kupigishwa magoti” na ubaya wa dhambi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana wawe ni mashuhuda wa imani tendaji inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwani ameshinda dhambi na mauti, mwaliko na changamoto ya kumkimbilia ili aweze kuwapatia nguvu ya kuipyaisha jamii ili iweze kusimikwa katika msingi thabiti wa haki na endelevu. Vijana wathubutu kujiaminisha mbele ya mwenyezi Mungu anayewawezesha kuwa ni vyombo vya upatanisho na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.