2017-09-08 16:29:00

Mchakato wa upatanisho wa upendo na kidugu!


Katika sala ya toba wakati wa adhimisho la ibada ya Misa Takatifu huwa tunaomba msamaha kwa nafasi mbalimbali za dhambi ikiwemo «kutokutimiza wajibu». Tendo hili la kutokutimiza wajibu linaonekana katika kuukimbia wajibu wetu au kubaki baridi katika mazingira mbalimbali ambayo yanatuhitaji kuwajibika kikristo. Moja ya maeneo hayo ni kukaa kimya au kutokumwongoza mwenzako ambaye anaelekea katika njia mbaya kurudi katika ukweli. Neno la Mungu katika Dominika hii linatuambia kwamba tunapoacha wajibu huo wa kupatana na kusahihishana kindugu yule anayepotea atakufa katika uovu wake lakini hatia yake inakuwa juu yako. Hivyo ni wajibu wetu kusahihishana na kurudishana katika njia ya ukweli.

Tunawajibika sababu ya mahusiano au muunganiko wa kindugu. Mara baada ya Tanganyika kupata Uhuru wake Mwalimu Nyerere alilihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa akionesha kutokuridhika kwake na kupitia yeye kwa Taifa zima la Tanganyika wakati huo kwa sehemu nyingine kutokupata Uhuru na kusema “hatuwezi kamwe kutoguswa na yanayoendelea kwa nchi nyingine ambazo zipo jirani na Tanganyika kwani matatizo yao ni matatizo yetu pia”. Kutokwenda sawa kwa mtu mwingine au kukengeuka kwa mtu mwingine kunapaswa kukuguse wewe kwani kwa nafasi ya kwanza tunao muunganiko wa kindugu. Sote tunaunganika kwa kuwa tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu lakini katika namna ya juu zaidi tumefanywa kuwa watoto wake warithi kwa njia ya Kristo.

Tunawajibika kwa sababu ni wajibu wetu wa kikristo wa kuwa wamisionari na kutafuta wokovu wa wote. Wewe mkristo unaitwa pia kuhangaikia wokovu wa mwenzako. Kristo anatutuma kwenda kuwafanya wote kuwa wafuasi wake, kwenda kuwatangazia wote habari njema ya wokovu. Habari hiyo ni msamaha na kuwatangazia maskini (wakosefu) Habari Njema ya wokovu wao. Kwa upande mwingine tunawajibishwa kwa sababu huenda nami nimechangia kuweka miundo mbinu katika kuanguka kwake, huenda nami nimefurahia au kufaidika katika uovu wake na nikawa kimya bila kukemea. Nionapo jirani yangu amepungukiwa katika njia moja au nyingine lazima nijihoji mchango wangu katika anguko hilo na hivyo nitapasika kurekebisha ili nami kufanya malipizi ya mchango wangu katika uovu wake.

Epuka kufanya ili kuondoa lawama. Kuna hatari ya kutimiza wajibu huu juu juu tu na kujikinai kwamba nimejitahidi lakini sikusikilizwa. Tunaalikwa kufanya kutoka moyoni na kunuia kwa manufaa yako na unayemsaidia. Kila mmoja anapaswa kuwa na dhamiri ya dhati kutoka moyoni ya kutaka kumrekebisha ndugu yake. Epuka kutenda ili kumkomoa mwingine. Njia ya kufuata inaelekezwa kupitia Kristo. Yeye anatuelekeza kwanza kuanza ndugu kwa ndugu, pili mbele ya shahidi mmoja au wawili na tatu mbele ya jumuiya. Mbinu zote hizi ni kunuia kufikia katika muafaka. Pengine kati yetu wawili tunaweza kuelewana na tusifikie hatua ya kuwashirikisha wengine lakini hali inapokuwa ngumu basi Hekima itumike na kuwafikia wengine lengo likiwa si kumuumiza mmoja kwa faida ya mwingine.

Lipo jambo la muhimu sana kuzingatia kabla ya kuanza hatua ya kumtafuta ndugu yako aliyepotea. Anza kwanza wewe kujisamehe. Msamaha na upatanisho lazima uanzie ndani ya nafsi yako. Si kufanya tu nje bila kuwa na msukumo wa ndani; hii ni kwa sababu msamaha unakurudishia ndugu yako ambaye unapaswa kujitoa kwake kikamilifu katika upendo wa kweli. Mara nyingi tunashindwa kutengeneza miundo mbinu ya uwezo wa msamaha na kujikinai kwamba mimi ndiye nimekosewa hivyo mkosaji aje kuomba msamaha. Lakini hatua kubwa na ya mwanzo ni ya wewe kusamehe kwanza moyoni hata kama hujaombwa msamaha. Anayesamehe kuanza moyoni anafungua milango kwa mkosaji kwenda kutafuta msamaha. Ni vigumu kuchota maji kwenye kisima ambacho mlango wake umewekewa kufuli zito. Jiweke tayari, tengeneza mazingira ya upatanisho na kaa na ndugu yako ili kurejeza tena undugu kati yenu.

Hatua hii ya kwanza inaposhindikana ndipo Kristo anapendekeza kushirikisha mtu mmoja au wawili. Hii haikusudii kumkomoa au kumtangaza mkosaji na aliyekosewa kujisafisha bali inakusudia kutafuta busara na maneno mbadala ya kutafuta suluhisho. Katika Maandiko ya Qumrani ilipendekezwa washirikishwe wazee ili kwa Hekima yao wawaongoze ndugu hawa wawili katika njia ya upatanisho. Mazingira haya yanarandana na namna walivyofanya jamii nyingi za kiafrika. Kanuni hapa inapaswa kuwa ni ile ile ya kutonuia kumkomoa mwingine au kumchafua mwingine kwa faida ya mwingine. Hatua ya tatu ya kushirikisha Jumuiya kubwa yaani Kanisa inanuia kupata mamlaka za kijamii ili kutoa maamuzi ya kijumla yatakayomtenga mmoja na jamii nzima.

Hapa twapaswa kutambua kwamba kutengwa huku si kwa namna ya kumfungia milango bali ni kutoa fursa na kujitafakari akiwa nje ya jamii. Kwa namna moja hapa tunaoneshwa kwamba sote katika jumuiya tunapaswa kutembea kama ndugu na tunaoongozwa na ndugu yetu mkubwa Kristo. Jamii hii ya Kanisa ambayo Kristo ameiunda inakwenda katika hali ya umoja na hivyo mmoja anapopingana na yanayosababisha umoja huo kimantiki anajitoa nje. Jamii hiyo imepatiwa na Kristo kama tulivyotafakari Dominika mbili zilizopita mamlaka ya kufungia pale linapoona inafaa, neno ambalo linajirudia hata leo hii pale anaposema: “yo yote mtakayoyafunga duniani, yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.”

Kwa maneno mengi hatupaswi kuogopa kumtenga anayekataa upatanisho wa kindugu, au anayekataa kurekebishwa. Katika somo la kwanza Mungu anatuambia kwamba ukimrekebisha nduguyo naye akang’ang’ania katika uovu wake basi atakufa katika uovu wake na hatia yake i juu yake. Nia ya dhati ya kurekebisha inanuia katika kujenga na si kubomoa na hivyo anayetaka kubaki katika uovu kimantiki anataka kubomoa na kwa busara anapaswa kutengwa na jamii iliyonuia kujenga. Mwaliko wa wimbo wa Zaburi katika Dominika hii ni katika kuisikiliza sauti ya Bwana. Tunaambiwa tusiifanye migumu mioyo yetu. Sauti yake inapenya kupitia ndugu zetu ambao wananuia kuturudisha katika mstari, kupitia jumuiya ambayo inahitaji uwepo wako.

Neno kubwa ambalo linapaswa kutawala mioyo yetu ni upendo kwa jirani zetu. Katika upendo, wote wawili, yaani anayerekebishwa na mrekebishaji watanuia katika mema. Hili ndilo analotuhasa Mtume Paulo kwamba si katika kuzishika amri bali upendo kwani upendo ndiyo utimilifu wa sheria. Tujivike upendo huo wa Mungu na kuwa tayari kutembea pamoja kindugu katika umoja huku tukielekea katika ukamilifu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.