Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Familia ya Mungu nchini Colombia twekeni hadi kilindini katika amani

Papa Francisko anaitaka familia ya Mungu nchini Colombia kutweka hadi kilindini ili kujenga amani na kutetea maisha!

08/09/2017 12:52

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Septemba 2017 alifunga siku ya pili ya hija yake ya kitume kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Simon Bolivar na kuhudhuriwa na bahari ya watu kutoka ndani na nje ya Colombia. Tukio hili limeongozwa na kauli mbiu “Wajenzi wa amani na watetezi wa maisha”. Amegusia dhamana na utume wa Mtakatifu Petro katika kuwaongoza ndugu zake kwenye ujenzi wa Ufalme wa Mungu; umuhimu wa kujiaminisha kwa Kristo Yesu, ili kweli waweze kuwa ni wajenzi wa amani na watetezi wa maisha!

Baba Mtakatifu amefafanua jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyobahatika kuwaita mitume wake wa kwanza kwa kuacha kazi ya uvuvi wa samaki baharini na kuanza kujikita kuvua watu! Bahari anasema Baba Mtakatifu, ni kielelezo cha dunia, mahali ambapo watu wote wanaishi, lakini wakati mwingine kuna nguvu zinazoweza kuhatarisha maisha ya viumbe hai duniani. Mwinjili Luka anaweka mbele ya Yesu bahari na umati mkubwa wa watu anayewashirikisha maneno ya haki, yenye kina na uhakika, kiasi cha kuwavuta watu wengi kuja kumsikiliza, ili hatimaye, waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Hili ni Neno linalowajalia watu usalama na uhakika wa maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema Bogotà, Colombia kama ilivyo miji mbali mbali ya dunia ina umati mkubwa wa watu na ardhi nzuri ambayo ingeweza kuzalisha mazao ili kukidhi mahitaji ya watu wengi zaidi. Lakini kuna nguvu zinazotishia maisha; kuna wingu kubwa la ukosefu wa haki msingi za binadamu na usawa; kuna rushwa na ufisadi; kuna utamaduni wa kifo unaotishia Injili ya uhai; kuna kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia, kuna vitisho vya ghasia, kichongo na kulipizana kisasi; kuna watu wanaojichukulia sheria mikononi mwao!

Katika mazingira kama haya, Yesu anamwambia Petro kutweka hadi kilindini! Hizi ndizo jitihada ambazo zimefanywa na wadau mbali mbali nchini Colombia katika mchakato wa kujenga amani na maridhiano. Kama ilivyokuwa kwa Petro Mtume, aliyejiaminisha kwa Yesu, akaacha yote na kumfuasa, akabahatika kuwa mvuvi mpya wa watu na utume wake ukawa ni kuwasaidia ndugu zake katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, mahali ambapo kuna furaha na utimilifu wa maisha. Hata nchini Colombia kuna watu walitambua dhamana ya kutweka hadi kilindini, ili kuwawezesha wananchi kujenga umoja na mshikamano ili kulinda na kutetea Injili ya uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Colombia inaweza kuwa ni nchi ambamo kuna haki, udugu pamoja na kusikiliza Neno la Mungu, changamoto kwa familia ya Mungu nchini Colombia kuendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishaji, kwa kumfuasa Kristo Yesu na kuonesha uwezo wa kupenda, kuthamini na kutetea maisha katika hatua zake zote. Mtakatifu Petro alitambua unyonge wake kama binadamu, lakini akajiaminisha kwa maneno na matendo ya Kristo Yesu; katika maisha na utume wake akaanguka, akasimama na kusonga mbele! Ndivyo ilivyo pia hata katika historia ya Colombia ambayo kwa bahati mbaya imeandikwa katika vita na ghasia; kinzani na mipasuko ya kijamii kiasi kwamba, si wote wamekuwa na ujasiri wa kujenga umoja wa kitaifa. Lakini, kama ilivyokuwa kwa Mtume Petro, hata leo hii, Yesu anawaalika wananchi wa Colombia kutweka hadi kilindini, kuthubutu na hatimaye, kuacha ubinafsi, woga na wasi wasi na kuanza kumfuasa ili kweli waweze kuwa ni wajenzi wa amani na watetezi wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

08/09/2017 12:52