Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko: sasa ni safari ya upatanisho na amani nchini Colombia

Papa Francisko anawashukuru wadau na wajenzi wa amani nchini Colombia, anaitaka serikali kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Kiinjili. - AP

07/09/2017 17:30

Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Colombia, Alhamisi, tarehe 7 Septemba 2017 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Colombia pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia. Katika hotuba yake amewashukuru wadau mbali mbali waliowezesha kukamilisha mchakato wa amani na maridhiano kati ya Serikali na Kikosi cha Mapinduzi ya Kijeshi “FARC”; ameitaka Serikali kukazia ustawi na maendeleo ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, Kanisa litaendelea na dhamana na utume wake wa kutangaza na kushuhudia amani, haki pamoja na kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anasema, hija hii ya kitume inayoongozwa na kauli mbiu “Demos el primer paso” yaani “Tupige hatua ya kwanza”, inafuata nyayo za watangulizi wake Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II. Lengo ni kushirikishana na familia ya Mungu zawadi ya imani na matumaini yatakayowawezesha watu wa Mungu kuvuka vikwazo na kuanza kujizatiti katika safari ya ujenzi wa Colombia inayopaswa kuwa ni nyumba ya wananchi wote pasi na ubaguzi. Colombia imebarikiwa na kukirimiwa na neema nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa maliasili na misitu pamoja na maeneo yenye kuvutia sana. Ina utajiri mkubwa wa watu wake wenye moyo wa upendo na ukarimu; watu wenye ujasiri wa kuweza kuvuka vikwazo na kusonga mbele!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, anapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wale wote waliowezesha kufanikisha mchakato wa amani na upatanisho; waliosaidia kukuza matumaini na amani; dhamana inayopaswa kutekelezwa na wote ili kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, licha ya shida, tofauti na kinzani zinazojitokeza! Jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa watu kukutana kwa kutoa kipaumbele cha kwa kwanza kwa utu, heshima na mafao ya wengi. Wananchi wote wajitahidi kuondokana na kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi au kujitafutia umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko na badala yake, wajielekeze zaidi katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani, kwa kuganga na kuponya madonda ya chuki na utengano, tayari kujenga madaraja ya udugu na kusaidiana!

Baba Mtakatifu anasema, kauli mbiu ya Colombia ni uhuru na nidhamu; mambo msingi yanayowawezeshsa watu kuishi kwa utulivu; kwa kuzingatia sheria sanjari na kujielekeza katika kubomoa miundo mbinu inayowatumbukiza watu katika umaskini wa hali na kipato! Ukosefu wa haki msingi za binadamu ni chanzo cha mipasuko na misiguano ya kijamii! Umefika wakati wa kuwapatia kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kutambua kwamba, tofauti zao ni utajiri mkubwa, kama alivyokazia Mtakatifu Petro Claver. Utu na heshima ya maskini, wanawake na watoto unapaswa kulindwa na kudumishwa, kwani wote hawa wanahitaji kwa ajili ya ujenzi wa matumaini nchini Colombia.

Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika kujenga na kudumisha haki, amani na mafao ya wengi mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Ni wajibu wa jamii kuheshimu uhai wa binadamu, kujenga jamii isiyokuwa na vita wala mipasuko ya kijamii; kwa kuzingatia tunu msingi za familia kadiri ya mpango wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, kulinda na kudumisha utu wao. Umefika wakati wa kuachana na vita, chuki, uhasama na hali ya kulipizana kisasi! Ni wakati wa safari ya kuelekea katika upatanisho na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

07/09/2017 17:30