Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Papa Francisko ni shuhuda wa upatanisho!

Papa Francisko ni chombo cha upatanisho kati ya watu! - AFP

07/09/2017 13:01

Askofu mkuu Óscar Urbina Ortega, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia, amemkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia kama kielele cha hija ya maisha ya kiroho ambayo yamefanywa na familia ya Mungu nchini Colombia ili kuwa tayari kupokea na kuumwilisha ujumbe na changamoto za Kiinjili zitakazotolewa na Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini Colombia. Huu ni mwaliko wa kuwa mashuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika umoja na upendo wa dhati!

Askofu mkuu Óscar Urbina Ortega kwa uchungu mkubwa anasikitika kusema, Colombia imepitia vipindi vigumu vya historia na maisha yake, kiasi hata cha kukosa hali ya kujiamini wenyewe na hivyo kuingiwa na kishawishi cha kukata tamaa pamoja na kuelemewa na mapungufu ya maisha! Lakini sasa, familia ya Mungu nchini Colombia inataka kuandika ukurasa mpya wa imani na matumaini kwa sasa na kwa siku za usoni. Anasema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao ni faraja na mwanga angavu.

Familia ya Mungu ncini Colombia ina hamu ya kusikiliza hekima inayofumbatwa katika maisha, utume na mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko ili kusaidia mchakato wa kufanya mang’amuzi, ili kuganga na kuponya madonda makubwa yaliyojificha katika sakafu ya mioyo yao. Baba Mtakatifu ni shuhuda na mjenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu waliogawanyika na kusambaratika kama umande wa asubuhi! Baba Mtakatifu ni shuhuda wa msmaha na upatanisho kati ya wananchi wa Colombia.

Colombia katika ujumla wake, inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kupiga hatua ya kwanza kama Kanisa ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu sanjari na kuimarisha tunu msingi zinazoimarisha haki, amani, upendo, udugu na mshikamano wa kitaifa kwa kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi. Lengo ni kusimama kidete kulinda, kudumisha na kutetea utu na heshima ya binadamu. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya familia ya Mungu nchini Colombia ni kuhakikisha kwamba, inakuwa ni chombo cha amani na upatanisho mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia linamshukuru Baba Mtakatifu kwa kukubali kupokea mwaliko wake, utakaoendeleza kazi ya ukombozi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

07/09/2017 13:01