Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Papa Francisko: Chemchemi ya huruma, upendo na upatanisho!

Papa Francisko ni chemchemi ya huruma, amani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu! - AFP

07/09/2017 12:39

Kardinali Rubèn Salazar Gomez, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bogotà, Colombia, anapenda kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili miongoni mwa familia ya Mungu nchini Colombia. Akiwa nchini humu, atafanikiwa walau kutembelea na kukutana na wananchi wa Colombia mjini Bogotà, Villavicencio, Medellìn pamoja na Cartegena. Colombia kwa sasa imeamua kuuvalia njuga mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, unaopania kuachana na kurasa chungu za vita, kinzani na mipasuko ambayo imewaachia wananchi wengi wa Colombia madonda makubwa ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; usawa, rushwa na ufisadi!

Familia ya Mungu nchini Colombia inataka kuandika ukurasa mpya wa amani, kwa kutengeneza mazingira ya upatanisho, haki endelevu, udugu na mshikamano; miundo mbinu itakayowezesha kujenga mafungamano ya kijamii, maendeleo sanjari na ugawaji sawa wa utajiri na rasilimali za nchi. Colombia inapania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, inaendeleza utamaduni, utajiri na tunu zake msingi, ili kuweza pia kuzishirikisha katika medani za kimataifa, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi.

Kumbe, anasema Kardinali Rubèn Salazar Gomez, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati pamoja na watu wa Colombia ni chachu muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Colombia mpya! Kanisa nchini Colombia nalo liko kwenye mchakato wa upyaisho wa maisha na utume wake! Wanatambua kwamba, Kanisa kwa hakika ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote. Kanisa linapania kujipyaisha kwa kuboresha maisha na utume wake kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu na wala si kwa kujikita katika uchu wa mali na madaraka; tabia ya kujitafuta na kupenda umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Colombia. Kanisa linataka kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wote.

Huu ni upendo anasema Kardinali Rubèn Salazar Gomez,  unao samehe, unaoponya, unaoalika na kuwaunganisha watu wote, ili waweze kujisikia kuwa watoto wa Baba mmoja, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu. Wanataka kutembea kwa pamoja, hadi kuyafikia maisha ya uzima wa milele. Ni matumaini ya Kanisa nchini Colombia kwamba, uwepo wa Baba Mtakatifu nchini mwao utasaidia kuendeleza mchakato wa upyaisho wa familia ya Mungu nchini Colombia. Haya ni maneno ambayo Kardinali Gomez ameyasema wakati wa kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia, tayari kuanza hija yake ya kitume kama hujaji wa amani na upatanisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

07/09/2017 12:39