2017-09-07 16:33:00

Familia ya Mungu nchini Kenya jengeni utamaduni wa utawala wa sheria


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika kipindi hiki kigumu cha historia ya nchi ya Kenya baada ya Mahakama kuu kubatilisha matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 Agosti 2017, lina waalika watu wa Mungu nchini Kenya kutofuatisha namna ya dunia hii, bali wageuzwe kwa kufanya upya nia zao, ili wapate kujua hakika ya mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. Maaskofu wanawataka wananchi wote wa Kenya kusimama kidete, ili kwa pamoja waweze kujenga nchi yao!

Baraza la Maaskofu Kenya linakishukuru Chama cha upinzani cha NASA kwa kufikisha malalamiko yake ya uchaguzi kwenye Mahakama kuu badala ya kesi hiyo kusikilizwa na kutolewa hukumu na raia mitaani, hali ambayo ingepelekea machafuko makubwa ya kisiasa nchini Kenya. Uamuzi huu umeiongezea Mahakama kuu sifa ya kuweza kutatua migogoro ya wananchi katika hali ya usalama na amani. Maaskofu wanawaalika wananchi wote wa Kenya kuzingatia utawala wa sheria kwa kukubali na kutekeleza maamuzi yaliyotolewa na Mahakama kuu. Uhuru, heshima na haki ya Mahakama kuu vinapaswa kuheshimiwa hata kama kimsingi mtu hakubaliani na maamuzi yaliyotolewa na Mahakama kuu.

Huu ndio utawala wa sheria na kwamba, hakuna sababu msingi ya kuendelea kuishambulia Mahakama wala kutoa vitisho kwa Majaji waliohusika katika kufikia uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu! Maaskofu wanampongeza Jaji Mkuu David Maraga kwa maamuzi aliyoyafanya na kwamba, sasa changamoto iliyoko mbele yao ni kushikamana ili kujenga taifa kwa kujikita katika nia njema. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawasifu na kuwapongeza wananchi wote waliojitokeza kupiga kura, kwa amani na utulivu na kuwataka tena kujitokeza kwa wingi wakati wa kupiga tena kura ya marudio hapo tarehe 17 Oktoba 2017.

Wananchi wa Kenya wanahimizwa kufanya kampeni za kistaarabu, zinazowajibisha, ili hatimaye, kuwapata viongozi watakaosukuma mbele gurudumu la maendeleo ya wananchi wote wa Kenya. Ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha kwamba, uchaguzi wa marudio unakuwa huru, wa haki na unaoaminiwa na wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linavialika vyama vyote kushirikiana na Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, IEBC sanjari na kuiachia uhuru wa kuweza kutekeleza majukumu yake pasi na kuingiliwa na wanasiasa. Badala ya kuishambulia Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya, wanasiasa watoe ushauri wa namna ya kuboresha utendaji wao wa kazi na kwamba, busara haina budi kutumika kwani si mambo yote yanaweza kufanyiwa marekebisho.

Maaskofu wanaunga mkono mchakato wa mabadiliko kwenye Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, IEBC ili kuwajengea wananchi imani katika mchakato mzima wa uchaguzi wa marudio hapo tarehe 17 Oktoba 2017. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linakaza kusema, litaendelea kusimamia mchakato wa kuimarisha taasisi, kukuza na kudumisha majadiliano sanjari na kuwa ni daraja la ujenzi wa amani, ili uchaguzi wa marudio uweze kuwa huru na wa haki mintarafu maamuzi ya Mahakama kuu. Maaskofu wanaendelea kuwasindikiza wananchi wote wa Kenya kwa  sala anasema, Askofu Philip Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika taarifa yake kwa vyombo vya habari. Hiki ni kipindi cha kushuhudia uzalendo, ili kuonesha kwamba akili na nyoyo zao kweli zimepyaishwa na kurekebishwa ili kujikita katika misingi ya haki, amani na ustawi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.